1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benitez afungashwa virago na Real Madrid

5 Januari 2016

Miamba ya ligi kuu ya Kandanda Uhispania Real Madrid imemtimua kocha wake Mhispania Rafael Benitez ambaye amehudumu miezi saba pekee.

https://p.dw.com/p/1HY1u
Rafa Benitez Trainer Real Madrid
Picha: picture-alliance/dpa/B. Alino

Sasa nafasi yake imechukuliwa na mchezaji wa zamani wa klabu hiyo na pia timu ya taifa ya Ufaransa Zinedine Zidane ambaye awali alikuwa Kocha wa Timu B ya Real Madrid.

Benitez ametimuliwa kufuatia kile kinachoonekana kuwa ni matokeo mabaya kwa timu hiyo, ambapo ilitoka sare ya magoli 2-2 na Valencia, katika Mechi ya La Liga, sare ambayo imewaacha vigogo hao nafasi ya 3 wakiwa nyuma ya viongozi wa ligi Atletico Madrid kwa pointi 4.

Tangu atue Madrid, Benitez amekuwa hapendwi na Mashabiki wa Klabu hiyo, baada ya kufungwa bao 4-0 kwenye mechi ya El Clasico mwezi Novemba na mahasimu wao Barcelona, pia kutupwa nje ya michuano ya Kombe la Mfalme maarufu kama Copa del Rey. Hii ni baada ya kumchezesha mchezaji asiyestahili katika mechi dhidi ya Cadiz.

Hali hiyo imefanya kuwepo minong'ono ya kila mara kuwa wachezaji wa Real Madrid hawana imani na mbinu za kocha huyo Mhispania na hivyo kuna kile kinachodhaniwa kuwa ni mgomo baridi dhidi yake.

Wiki iliyopita Benitez aliwatuhumu wanahabari kwa kuendesha kampeni ya kumpinga yeye, klabu na rais wao Florentino Peréz.

Mwandishi: Sekione Kitojo/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef