1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bemba ahukumiwa miaka 18 jela

Sylvia Mwehozi21 Juni 2016

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu The Hague imemhukumu kifungo cha miaka 18 jela, aliyekuwa makamu wa zamani wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Jean-Pierre Bemba, kwa makosa ya uhalifu wa kivita.

https://p.dw.com/p/1JAP6
Niederlande Kongo Jean-Pierre Bemba Gombo wegen Kriegsverbrechen in Den Haag verurteilt
Picha: picture-alliance/dpa/EPA/M. Kooren
Aliposoma hukumu hiyo, Jaji Silvia Steiner, amesema kiongozi huyo wa zamani wa wanamgambo alishindwa kulidhibiti jeshi lake la binafsi ambalo alilituma kwenda nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati mnamo Oktoba 2002 ambako walifanya vitendo vya kikatili vya ubakaji, mauaji na uporaji wa kikatili.

Bemba ni afisa wa ngazi ya juu kuhukumiwa katika mahakama hiyo ya ICC baada ya kupatikana na hatia mwezi Machi kwa mashitaka matano ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu. Hii ni adhabu kubwa na ya kwanza ya mahakama hiyo kutolewa dhidi ya kiongozi wa juu.

Hatia ya makosa

Alihukumiwa hapo Machi kwa makosa matano ya uhalifu wa vita na uhalifu wa kibinadamu, baada ya kutuma kikosi cha askari 1500 kutoka katika jeshi lake binafsi kwenda Afrika ya kati katika kile kinachodaiwa kusaidia kufanya mapinduzi dhidi ya rais wa wakati huo wa nchi hiyo.

Askari wa jeshi lake binafsi wanadaiwa kutekeleza ubakaji na mauaji na kudaiwa kushiriki mapinduzi ya rais Ange-Felix Patasse.

Mwendesha mashitaka mkuu wa ICC Fatou Bensouda
Mwendesha mashitaka mkuu wa ICC Fatou BensoudaPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Lampen

Wataalamu walithibitisha kwamba matukio hayo ya ukatili yangeleta athari za muda mrefu kwa jamii na waathirika wenyewe.

Katika hukumu iliyotolewa mwishoni mwa kesi hiyo iliyoanza mwezi Novemba mwaka 2010, majaji wa mahakama ya ICC waliona kwamba licha ya kufahamu kile kilichokuwa kikiendelea, Bemba alishindwa kuchukua hatua zozote za kuzuia aina yoyote ya uhalifu, ikiwemo magenge ya ubakaji wa wanaume, wanawake na watoto, wakati mwingine ndugu zao wakilazimishwa kuangalia.

Wanaharakati walisema hukumu ya miaka 25 iliyopendekezwa awali na waendesha mashitaka haikulingana na uzito wa makosa yanayomkabili.

Mahakama hiyo iliwahi kutoa hukumu ya miaka 14 na 12 gerezani kwa washitakiwa wengine wawili.

Pamoja na kulichukulia suala la ubakaji kama silaha ya kivita, Kesi ya kiongozi huyo pia imekuwa ya kwanza katika mahakama ya ICC kumlenga moja kwa moja kamanda wa kijeshi kwa makosa yaliyofanywa na askari wake, hata kama hakutoa amri yoyote.

Mawakili upande wa utetezi wanadai kwamba Bemba ambaye amekuwa kizuizini kwa miaka nane tangu kukamatwa kwake mwaka 2008 mjini Brussels, alipaswa kuachiwa.

Mahakama ya kimataifa ya The Hague
Mahakama ya kimataifa ya The HaguePicha: picture-alliance/AP Images/J. Lampen

Mmoja wa mawakili Peter Haynes aliiambia mahakama hiyo mwezi uliopita kuwa "Bemba hakushiriki katika makosa hayo. Hakuwepo kutoa amri wala kuwahamasisha askari wake" alisema kwamba hata hakuwepo katika nchi yalikofanyika makosa hayo.

Wanaharakati hata hivyo walionya kwamba hukumu nyepesi itashindwa kutoa onyo kwa makamanda wengine wa kijeshi

"Ni muhimu kwa mahakama kutambua wajibu wa kamanda, na kuna nafasi ya kuzuia" alisema Carrie Comer mwakilishi wa kudumu wa ICC kwa Shirikisho la Kimataifa la Haki za Binadamu (FIDH).

"Kama alijua au angefahamu, mambo haya yalitokea na yeye ndio mdhibiti mkuu kwa kikosi cha jeshi, ndio, anawajibika kabisa kwa kutozuia au kuwaadhibu waliotenda makosa hayo" anasema mwanaharakati huyo.

Kesi hiyo ya Bemba iliwashangaza wengi kwa kuchukua muda mrefu kutambua uhalifu wa ngono katika mahakama ya kimataifa.

Mwandishi:Sylvia Mwehozi/AFP

Mhariri:Saumu Yusuf