Beirut:Wanajeshi zaidi wa Ufarnsa wawasili Lebanon.
25 Agosti 2006Kundi jengine la wanajeshi wa kifaransa 170 wamewasili huko kusini mwa Lebanon katika mji wa Naqura.
Wanajeshi hao watakuwa chini ya uongozi wa majeshi ya kimataifa katika maeneo ya mpaka pamoja na wanajeshi wa Israel.
Hili limekuja saa moja kabla ya mawaziri wa masuala ya kigeni wa Umoja wa Ulaya kukutana huko Brussels nchini Ubelgiji kuzungumzia uwezekano wa kuongeza majeshi ya Umoja wa Mataifa huko kusini mwa Lebanon.
Katika mkutano huo pia unatazamiwa kuhudhuriwa na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan.
Rais wa Ufaransa Jacques Chirac ametangaza kuwa nchi yake itachangia jumla ya wanajeshi 2,000 katika jeshi hilo la kulinda amani.
Rais Chirac ameelezea masharti yaliyopelekea uamuzi huo uliochukuliwa kwa kusema.
„ Hivi sasa masharti yaliyowekwa na Ufaransa yametimizwa. Kuweko na maafikiano juu ya kiwango cha mchango kinachohitajika kwa kila nchi“.
Ufaransa imekuwa ikilaumiwa kwa uwamuzi wake wa kuchangia wanajeshi 200 tu katika jeshi la kulinda amani kusini mwa Lebanon.
Nchi hiyo imeongeza idadi yake hivi sasa baada ya Italia kutangaza kuchangia wanajeshi 3,000 na kuwa radhi kuliongoza jeshi hilo litakalokuwa na wanajeshi 15,000.
Wakati huo huo rais wa Ufaransa Jacques Chirac hapo baadae hii leo atakuta na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel mjini Paris nchini Ufaransa ambapo suala la kutumwa wanajeshi wa kulinda amani nchini Lebanon ndio mada kuu ya mkutano wao huo.