Beirut:Condoleezza Rice aitembelea Lebanon.
24 Julai 2006Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani bibi Condoleezza Rice amewasili Beirut bila ya kutarajiwa wakati mapigano yakiendelea kati ya jeshi la Israel na wanamgambo wa Hezbollah.
Maafisa wa Marekani wamesema, safari ya Condoleezza Rice huko Beirut ni kuonyesha jinsi gani anawaunga mkono wananchi wa Lebanon.
Mapema alitaka kusitishwa kwa mapigano, huko kusini mwa Lebanon, lakini akionya kuwa makubaliano yoyote lazima yawe ya kuivunja nguvu Hezbollah na kuiwezesha Lebanon kuwa na mamlaka yake kamili.
Bibi Condoleezza Rice baada ya kumaliza mazungumzo yake na viongozi wa Lebanon, pia atasafiri hadi Jerusalem kwa mazungumzo na Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert.
Jeshi la Israel limethibitisha kuanguka kwa helikopta yake huko kaskazini mwa Israel iliyotunguliwa na wanamgambo wa Hezbollah.
Katika mashambulizi hayo ya siku 13 yanayofanywa na vikosi vya kijeshi vya Israel na wanamgambo wa Hezbollah, tayari yameshasababisha vifo vya wa- Lebanon 362, na wa- Israel 37 wengi wao wakiwa raia wa kawaida.