1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIRUT: Wanajeshi wa Hispania wawasili Lebanon

15 Septemba 2006
https://p.dw.com/p/CDBz

Mamia ya wanajeshi wa Hispania wamewasili katika pwani ya kusini mwa Lebanon hii leo kujiunga na kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani.

Kamanda wa kikosi cha Umoja wa Mataifa, jenerali Alain Pellegrini, kutoka Ufaransa, amesema hakuna nafasi ya kuwaweka wanajeshi wanaondelea kuwasili. Amewakumbusha maofisa wa serikali ya Lebanon watoa nafasi zaidi, jambo ambalo mpaka sasa hawajalifanya.

Wakati huo huo, rais Geoerge W Bush wa Marekani amesema mzozo wa Lebanon ni sehemu ya vita kati ya uhuru na ugaidi unaojitokeza katika eneo zima la Mashariki ya Kati. Magaidi na wadhamini wao wanafahamu kwamba eneo la Mashariki ya Kati linapitia wakati mgumu katika historia yake.

´Uhuru umeleta matumaini kwa mamilioni ya watu na umesaidia kudumisha demokrasia changa toka Baghdad hadi Beirut. Lakini demokrasia hizi changa bado zinalegalega. Magaidi wanaogopa kukua kwa demokrsia kwa sababu wanajua ina maana gani kwa itikadi yao katika siku za usoni. Tutawashinda magaidi kwa kuzisaidia demokrasia changa za Mashariki ya Kati.´

Rais Bush amesema sio sadfa kwamba mataifa mawili yanayojenga jamii huru katikati mwa Mashariki ya Kati, Lebanon na Irak, ni mataifa kunakotokea mashambulio mabaya zaidi ya kigaidi.