BEIRUT. Vikosi vya mwisho vya wanajeshi wa Syria vyaondoka Lebanon.
25 Aprili 2005Vikosi vya mwisho vya wanajeshi wa Syria vimeondoka kutoka Lebanon mapema leo hivyo kumaliza miaka 29 ya kulikalia taifa hilo jirani. Mamia ya wanajeshi walichoma stakabadhi, kubomoa kuta na kuifukia mitaro wakati walipokuwa wakiondoa kutoka vituo vyao, katika bonde la Bekaa, mashariki mwa nchi hiyo.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Israel, Silvan Shalom, amesema Israel ina matumaini kwamba kuondoka kwa wanajeshi wa Syria kutoka Lebanon kutaifungulia milango amani mjini Beirut.
Wakati huo huo, kiongozi wa usalama mwenye usemi mkubwa nchini Lebanon, na anayeegemea upande wa Syria, Jamil al-Sayyed, amewasilisha barua ya kutaka kujiuzulu kutoka kwa wadhifa wake, muda mfupi kabla ya vikosi vya Syria kuondoka nchini humo. Alisema yuko tayari kujiuzulu wakati wa uchunguzi wa kifo cha waziri mkuu wa zamani Rafiki Hariri ulioitishwa na umoja wa mataifa.