BEIRUT: Uhalifu wa vita wadaiwa kufanyika Lebanon
11 Agosti 2006Kundi la kutetea haki za binaadamu la Human Right Watch limechapisha repoti yenye kushutumu Israel pamoja na Hezbollah kwa kuwalenga raia kiholela katika mashambulizi yao yanayoendelea.
Nodim Houry ambaye anaongoza tawi la shirika hilo nchini Lebanon ameiambia Deutsche Welle kwamba uchunguzi wa kimataifa unahitajika kuangalia uwezekano wa vitendo vya uhalifu wa vita.
Katika matukio mengine mashirika ya misaada yameonya kwamba hospitali kusini mwa Lebanon zimekuwa zikiishiwa na madawa,chakula na mahitaji megine muhimu kwa haraka ikiwa ni matokeo ya mapigano hayo kati ya Israel na Hezbollah.
Mashirika ya misaada yamesema hayawezi kuwafikia watu 100,000 wanaohitaji misaada kutokana na kupigwa marufuku na Israel nyendo zozote zile katika eneo hilo pamoja na kukataa kwake kuhakikishia usalama misafara ya magari ya misaada.