BEIRUT : Syria kuhamisha vikosi vyake Lebanon Jumatatu
6 Machi 2005Syria itaanza kuhamisha vikosi vyake nchini Lebanon kwa kuvipeleka bonde la Bekaa hapo kesho.
Waziri wa Ulinzi wa Lebanon Abdul Rahim Mrad ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba vikosi hivyo vitarudishwa nyuma kutoka Labenon ya Kaskazini na Mlima Lebanon kwa kuzingatia makubaliano ya Taif ambayo yalikomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe vya nchi hiyo kuanzia mwaka 1975 hadi mwaka 1990.Amesema kuhamishwa kwa vikosi hivyo kutaanza kutekelezwa mara moja baada ya mkutano wa Marais wa nchi hizo mjini Damascus kuidhinisha mpango wa kuondolewa kwa vikosi vya Syria nchini humo kulikotangazwa hapo jana na Rais Bashar al Assad.
Makundi yanayoiunga mkono Syria yamekataa kujitowa haraka na kwa vikosi vyote vya Syria vilioko Lebanon kwa sababu ya kile ilichosema nchi hiyo bado iko katika hali ya vita na Israel.
Kiongozi wa kundi la Hezbollah nchini Lebanon Sheikh Hassan Nasrallah amesema wanapinga kuwekwa kwa wanajeshi hao kwenye bonde la Bekaa nchini Lebanon kwa kuzingatia Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nambari 1559 ambalo linataka kuondolewa kwa wanajeshi hao wa Syria haraka na kwa ukamilifu.