BEIRUT: Steinmeier aliunga mkono pendekezo la Lebanon
9 Agosti 2006Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, ameliunga mkono pendekezo la Lebanon la kupeleka wanajeshi elfu 15 kulinda amani kati ya wanamgambo wa Hezbollah na jeshi la Israel, kusini mwa nchi hiyo.
Baada ya mazungumzo yake na waziri mkuu wa Lebanon, Fuad Siniora, juu ya pendekezo la azimio la Umoja wa Mataifa, Stenmeier amesema Ujerumani ina hofu juu ya idadi kubwa ya wakimbizi waliolazimika kuzihama nyumba zao kwa sababu ya mapigano.
Waziri Steinemer tayari amewasili nchini Israel ambako waziri mkuu wa nchi hiyo, Ehud Olmert, amesema analichunguza pendekezo la Lebanon kutuma wanajeshi katika eneo la kusini.
Wanadiplomasia katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani wanasema Ufaransa imekuwa ikiishawishi Marekani ilikubali takwa la Lebanon linaloitaka Israel iwaondoe wanajeshi wake kutoka kusini mwa nchi hiyo.
Israel inasema itawaondoa wanajeshi wake mara tu kikosi cha kimataifa kitakapopelekwa kusini mwa Lebanon.