1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIRUT: Serikali ya Lebanon yajiondoa mamlakani.

1 Machi 2005
https://p.dw.com/p/CFaQ

Waziri mkuu wa Lebanon Omar Karami amelazimika kujiuzulu pamoja na serikali yake kufuatia upinzani mkali.

Hali hii ni kutokana na upeo wa mgogoro wa kisiasa nchini Lebanon baada ya kifo cha aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo Rafik Hariri katika wiki mbili zilizopita.

Kutangazwa kujiuzulu kwa serikali ya waziri mkuu Omar Karami kulitekelezwa wakati bunge la nchi hiyo lilipokuwa likiendelea na mada nyeti iliyowasilishwa bungeni na upande wa upinzani ya kutokuwa na imani na uongozi wa nchi hiyo.

Vyama pinzani nchini humo vimekuwa vikielekeza lawama kwa serikali ya Lebanon ambayo ina ushirikiano wa karibu na Syria kwa mauaji ya aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo Rafik Hariri.

Habari za kujiuzulu kwa serikali ya Lebanon zilipokelewa kwa shangwe na nderemo na maelfu ya watu ambao waliandamana katikati mwa mji wa Beirut.

Kumekuwa na maandamano kuipinga serikali na kuitaka Syria iachane na mambo ya ndani ya Lebanon hata baada ya serikali kuharamisha maandamano hayo.