1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Beirut: Mashambuliano baina ya Israel na Hizbullah yanaendelea huko Lebanon.

23 Julai 2006
https://p.dw.com/p/CBIi

Ikiwa ni siku ya kumi na mbili mfululizo, majeshi ya Israel yameyashambulia kwa mabomu maeneo ya mji mkuu wa Libanon, Beirut, na sehemu za kusini mwa nchi hiyo. Pia mji wa bandari wa Sidon ulipigwa, na watu watatu walijeruhiwa. Maeneo ya Bonde la Bekaa pia yalishambuliwa na viwanda vitatu vikaharibiwa. Kwa mujibu wa habari ni kwamba jeshi la Israel limeteka maeneo yalio muhimu, kijeshi, katika mpaka baina nchi hizo mbili.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, ameionya Israel isiivamie Lebanon. Alisema anafikiri jambo hilo litakuwa la hatari sana kuupanua mzozo huo. Bila ya shaka yatazidi mapigano baina yao na Hizbullah. Ikiwa watabaki huko na kukusudia kile walichokiita hapo zamani ukanda wa amani, huo utakuwa ukanda wa amani kwao, lakini kwa wengine itamaanisha ardhi yao imetekwa. Na jambo hilo litazidisha upinzani.

Pia mashambulio ya maroketi ya Chama cha Hizbullah cha Libanon na ya Wapalastina wenye siasa kali dhidi ya Israel yanaendelea. Hadi sasa katika vita hivyo wamekufa Wa-Libanon 350, wengi wao wakiwa ni raia. Mashambulio ya Chama cha Hizbullah yamewauwa Wa-Israeli 35.

Wakuu wa Cyprus wanatarajia kuwasili katika nchi yao wakimbizi wengine 10,000 kutokea Libanon. Mnamo masaa yajayo, inatarajiwa meli 14 zitawasili katika bandari za Larnaca na Limassol. Umoja wa Mataifa umetoa mwito wa kutolewa dola milioni 100 kwa ajili ya wakimbizi walioko ndani ya Libanon.

Na wizara ya mambo ya kigeni ya Ujerumani mjini Berlin imetoa ilani kwamba raia wa Kijerumani na wa nchi nyingine za Umoja wa Ulaya ambao bado wako Kusini mwa Libanon wanaweza kesho kusafirishwa kwa meli iliokodiwa kutokea Libanon kwenda Cyprus. Na kutoka hapo tayari ziko ndege za kuwasafirisha hadi nchi zao. Watu hao wanatakiwa wakusanyike katika nyumba ya mapumziko ilioko Tyrus, Sur.