BEIRUT: Mapigano yazuka tena kaskazini mwa Lebanon
28 Mei 2007Matangazo
Makubaliano ya kusitisha mapigano kaskazini mwa Lebanon ambayo hayakuwa rasmi, yamevunjika huku mapigano yakizuka tena baina ya jeshi la Lebanon na wanamgambo kwenye kambi ya wakimbizi wa kipalestina.
Milio ya risasi ilisikika ndani ya kambi ya wakimbizi ya Nahr al Bared huku makundi ya kipalestina, yakiwemo Fatah na Hamas, yakijaribu kufikia suluhisho la kisiasa kumaliza mapigano hayo.
Wanajeshi wa Lebanon wameizingira kambi hiyo ya wakimbizi na inasemekana wanapania kuizingira kwa muda mrefu.
Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema zaidi ya wakimbizi elfu 20 wameikimbia kambi ya Nahr al Bared tangu machafuko yalipozuka wiki moja iliyopita, lakini maelfu bado wamekwama ndani ya kambi hiyo.