BEIRUT: Mapigano yaendelea Lebanon na Gaza
27 Julai 2006Ndege za Israel zimendelea na mashambulio yake usiku wa leo nchini Lebanon na katika Ukanda wa Gaza.Mashambulio hayo yamelenga kituo cha jeshi la Lebanon kaskazini mwa mji mkuu Beirut na mnara wa matangazo ya redio karibu na eneo hilo. Wanamgambo wa Hezbollah na majeshi ya Israel yamepambana vile vile kusini mwa Lebanon, ikisemekana kuwa hayo ni mapigano makali kabisa kutokea tangu Israel kuanza kuishambulia Lebanon majuma mawili yaliyopita.Si chini ya wanajeshi 9 wa Israel wameuawa na wengine 25 wamejeruhiwa.Katika mji wa Tyre kusini mwa Lebanon,makombora ya Israel yameteketeza jengo la ghorofa lililokuwa na ofisi za kamanda mkuu wa Hezbollah.Wapiganaji wa Hezbollah vile vile wamerusha makombora mengine kaskazini mwa Israel na kuwajeruhi watu wengi.Kwa upande mwingine mashambulio ya Israel katika Ukanda wa Gaza,yameua Wapalestina 23.Miongoni mwao ni mwanamgambo mmoja wa kundi la Islamic Jihad na wafuasi wa kundi la Hamas linaloiongoza serikali ya Kipalestina.