BEIRUT: Mapigano mapya yazuka nchini Lebanon.
24 Mei 2007Mapigano mapya yamezuka kati ya majeshi ya Lebanon na wanamgambo wa kiislamu ambao tangu siku ya Jumapili iliyopita wamejificha katika kambi ya wakimbizi ya wapalestina nchini humo.
Wakazi wengi wa kambi hiyo wamekimbia ingawa maelfu ya wakimbizi bado hawajaondoka.
Wanamgambo kadha walijaribu kutoroka wakitumia mashua mbili, lakini kikosi cha wanamaji wa nchi hiyo kikazishambulia na kuzizamisha mashua hizo.
Waziri Mkuu wa Lebanon, Fouad Siniora, amesema serikali yake haitatetemeshwa na magaidi na kwamba itakabiliana vilivyo na ugaidi.
Mkesha wa kuamkia leo watu kumi na sita walifariki dunia baada ya shambulio la bomu katika mji wa Aley karibu na mji mkuu, Beirut.
Hilo ndilo shambulizi la tatu kutekelezwa kiasi siku nne zilizopita.
Kundi la Fatah al-Islam, linalopambana na majeshi ya serikali katika kambi ya wakimbizi ya Nahr al-Barid, limesema halijahusika na mashambulio yao.