BEIRUT: Magazeti ya Lebanon yaikosoa Marekani
27 Julai 2006Magazeti ya mjini Beirut nchini Lebanon yameikosoa Marekani kwa kuuvuruga mkutano wa mjini Roma Italia ambao walebanon walitumaini ungetoa mwito wa kusitishwa mapigano kati ya Israel na kundi la Hezbollah.
Gazeti la As Safir katika ukurasa wake wa kwanza limeandika, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Condoleezza Rice anaendelea kuupiga risasi na kuua mkutano wa Roma.
Nalo gazeti la An Nahar limeandika, malumbano ya Ulaya na Marekani yauvuruga mkutano wa Roma. Gazeti hilo limesema mashambulio ya jana ya Hezbollah yamesababisha mshutuko mkubwa kwa kisiasa na kijeshi nchini Israel.
Mkutano wa mjini Roma ulishindwa jana kufikia makubaliano ya kuyasitisha mapigano ya wiki mbili kati ya Israel na Hezbollah. Hata hivyo wanadiplomasia kutoka Ulaya, Marekani na mataifa ya kiarabu walikubaliana juu ya umuhimu wa kupeleka kikosi cha kimataifa kusini mwa Lebanon chini ya mamlaka ya Umoja wa Mataifa.
Akizungumza baada ya mkutano huo waziri mkuu wa Lebanon, Fuad Siniora alisema, ´Inatupasa kushirikiana ili kufikia usitiswaji wa mapigano utakaoweza kuilinda Lebanon na kuiwezesha kupata ardhi yake. Na hiyo itairuhusu serikali ya Lebanon kuwa na usemi nchini kote na hakutakuwa na silaha nje ya mamlaka ya serikali halali.´
Ufaransa inataka mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ufanyike wiki ijayo kuutanzua mzozo wa Lebanon.
Waziri wa sheria nchini Israel Haim Ramon amesema leo kwamba mkutano wa mjini Roma uliipia Israel ruhusa ya kuendelea na harakati yake ya kijeshi mpaka wanamgambo wa Hezbollah waondolewe kusini mwa Lebanon.