BEIRUT: Lebanon yaomboleza mbunge aliyeuawa.
14 Juni 2007Lebanon inaadhimisha siku ya kitaifa ya maombolezi kutokana na mauaji ya mbunge Walid Eido anayeipinga Syria.
Mbunge huyo alifariki dunia pamoja na mwanawe na watu wengine wanane baada ya shambulio la bomu lililotegwa kwenye gari.
Walid Eido, ambaye amezikwa leo baada ya swala ya adhuhuri, ni miongoni mwa watu kadha wanaoipinga Syria waliouawa nchini Lebanon tangu mwaka 2005 wakati waziri mkuu wa zamani, Rafiki al-Hariri alipouawa.
Waziri Mkuu wa Lebanon, Fouad Siniora ametoa wito wa kuandaliwa kikao cha dharura cha Umoja wa Mataifa ya Kiarabu.
Jumuiya ya kimataifa imeshutumu shambulio hilo.
Syria imekanusha kwamba inahusika.
Mhariri Mkuu wa gazeti la An Nahar nchini Lebanon, Edmond Saab amezungumzia mauaji hayo:
"Awali tuliuzingatia uhalifu huo kwa misingi ya mauaji yaliofanywa siku za nyuma dhidi ya wanaharakati wanaoipinga Syria. Tumeishutumu Syria kwa mauaji hayo. Hata hivyo hakuna ushahidi wowote kwa kuwa uchunguzi haujafanywa. Kwa hali ilivyo nchini Lebanon kuna uwezekano wa makundi mengi kuhusishwa. Hivi karibu kuna watu ambao wanashuku yamkini kundi la al-Qaeda limehusika. Pia wengine wanashuku huenda mauaji hayo yana uhusiano na vita vinavyoendelea kati ya majeshi na wanamgambo wa Kiislamu kaskazini mwa nchi"