BEIRUT: Lebanon yaendelea kushambuliwa na Israel
17 Julai 2006Israel imeendelea na mashambulio yake ya kijeshi nchini Lebanon kwa siku ya tano.Mashambulio ya angani kwa mara nyingine tena yamelenga uwanja wa ndege wa kimataifa wa Beirut na vituo vya Hezbollah kusini mwa Lebanon.Katika kijiji kimoja kusini mwa nchi,wakazi 8 waliuawa baada ya jengo moja kushambuliwa kutoka angani.Duru za Lebanon zimesema,watu wasiopunga 19 wameuawa na zaidi ya 50 wamejeruhiwa baada ya vituo vya kijeshi vya Lebanon kushambuliwa kwa mabomu katika mji wa bandari wa Tyre.Ukanda wa Gaza vile vile umeshambuliwa na Israel.Katika mashambulio hayo jengo la wizara ya mambo ya kigeni ya Wapalestina limepigwa bomu kwa mara ya pili katika kipindi cha juma moja.Wale walioshuhudia shambulio wamesema,sehemu moja ya jengo hilo la ghorofa nane iliporomoka;na watu 5 waliokuwa karibu walijeruhiwa.Israel inasema kuwa wanamgambo wa Hamas hutumia jengo hilo kupanga mashambulio yao.