BEIRUT :Lebanon yaelekea katika machafuko mapya?
11 Machi 2005Rais wa Lebanon hapo jana amemteuwa tena Waziri Mkuu anayeiunga mkono Syria Omar Karami na kuhatarisha kuzuka kwa malumbano mapya na upinzani ambayo yalimlazimisha mwanasiasa huyo wa madhehebu ya Sunni kujiuzulu siku 10 zilizopita.
Karami ambaye alijiuzulu kutokana na maandamano makubwa dhidi ya Syria mjini Beirut amesema lengo lake jipya hivi sasa ni kuunda serikali ya umoja wa kitaifa nchini Lebanon.Baraza lake la mawaziri lililopita lilikuwa limejaa mawaziri wanaoiunga mkono Syria.
Wakati huo huo wanajeshi wa Syria wamekuwa wakiendelea kuelekea mashariki mwa nchi hiyo kwa kutekeleza makubaliano ya mpango wa kuviondowa vikosi hivyo kwa awamu mbili ambayo yamefikiwa wiki hii mjini Damascus na waziri wa ulinzi wa Lebanon anasema wengine maelfu tayari wameanza kuelekea mpakani mwa nchi hiyo.
Upinzani nchini Lebanon unataka kukomeshwa kwa ushawishi wa Syria katika ngazi zote nchini humo.