BEIRUT : Kikosi cha Italia chawasili kulinda amani
2 Septemba 2006Vikosi vya Italia vimewasili nchini Lebaon kuimarisha usitishaji wa mapigano kati ya Israel na kundi la wanamgambo wa Kishia la Hizbollah unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa.
Msemaji wa kijeshi amesema wanajeshi hao wataendesha shughuli za upepelezi kabla ya kuwekwa kwa kikosi kamili cha wanajeshi 800 kusini mwa Lebanon.Italia inakusudia kuweka wanajeshi 2,500 wa ardhini katika awamu mbili kwenye kipindi cha miezi minne na kupelekea kuwa na mchango mkubwa kabisa katika kikosi hicho cha kimataifa cha kulinda amani.
Wanajeshi hao wa kulinda amani wanatakiwa walisaidie jeshi la Lebanon wakati likiwekwa hadi kwenye mpaka na Israel wakati wanajeshi wa Israel wakiondoka katika ardhi ya Lebanon.
Mataifa ya Ulaya yameahidi kutowa zaidi ya wanajeshi 7,000 wakiwemo wanajeshi 2,000 kutoka Ufaransa.