BEIRUT: Israel yafanya mashambulio makubwa kusini mwa Lebanon
27 Julai 2006Israel imefanya mashambulio makubwa ya angani na ya ardhini kusini mwa Lebanon, kufuatia kuuwawa kwa wanajeshi wake tisa kwenye mapigano mabaya zaidi kuwahi kutokea katika mgogoro wa siku 16 kati ya Israel na kundi la Hezbollah.
Ndege za Israel zimeviharibu vituo vya redio kaskazini mwa mji wa Beirut na kuyashambulia malori matatu yaliyokuwa yamesheheni chakula na madawa yakielekea eneo la mashariki mwa Lebanon. Duru za usalama nchini Israel zinasema madereva wawili wa malori hayo wameuwawa.
Wapiganaji wa kundi la Hezbollah wamevurumisha maroketi kaskazini mwa Israel, ikiwa ni pamoja na mji wa Haifa, na kuwajeruhi watu kadhaa.
Chakula, umeme na madawa yamekatizwa huku walebanon takriban elfu 800 wakiwa wamepoteza makaazi yao. Shirika la kutoa misaada ya kiutu la Umoja wa Mataifa limeonya juu ya ukosefu mkubwa wa chakula.