BEIRUT : Israel yaendelea kushambulia Lebanon
10 Agosti 2006Vikosi vya Israel na Hezbollah vinaendelea kupambana wakati vikielekea kwenye mji wa kusini wa Khiam nchini Lebanon.
Mashambulizi ya anga ya Israel na mizinga tayari yamekuwa yakiushambulia mji huo.Mapema wanajeshi wa ardhini wa Israel walisonga mbele na kuichukuwa miji ya Wakristo ya Marjayun na Qlaiah bila ya upinzani..Hata hivyo maafisa wa kijeshi wa Israel wamesema huo sio mwanzo wa kutanuwa mashambulizi ya Israel kwa Lebanon hatua ambayo imeiidhinishwa na baraza la mawaziri la Israel hapo jana.
Mashambulizi ya anga ya Israel pia yameupiga mnara wa radio uliokuwa hautumiki kwenye mji mkuu wa Beirut. Duru za Lebabon zinasema shambulio hilo ni la ndani kabisa kwenye mji mkuu tokea mashambulizi hayo yaanze mwezi mmoja uliopita.
Wakati huo huo wapiganaji wa Hezbollah wamekuwa wakiendelea kuvurumisha maroketi kaskazini mwa Israel ambapo watu wawili wameuwawa akiwemo mtoto mchanga.