BEIRUT: Israel yaendelea kuishambulia Lebanon
14 Julai 2006Israel imeimarisha mashambulio yake nchini Lebanon,ndege za kivita zikilenga vitongoji kusini mwa mji mkuu Beirut,eneo linalosemekana kuwa ni ngome ya wanamgambo wa Hezbollah.Ndege zimeshambulia mtambo wa umeme,barabara inayoelekea uwanja wa ndege wa Beirut na barabara kuu ya Beirut kuelekea mji mkuu wa Syria, Damascus.Mashambulio hayo yamefanywa siku moja baada ya Israel kuziziba bandari zote nchini Lebanon na kubomoa uwanja wa ndege wa Beirut ambao sasa hauwezi kutumika.Ripoti zasema,zaidi ya watu 50 wameuawa nchini Lebanon.Wakati huo huo,mashambulio ya makombora yaliyofanywa na wapiganaji wa Hizbollah kaskazini mwa Israel, yamewauwa raia 2 wa Kiisraeli.Makombora mawili yaliangukia mji wa bandari wa Haifa.Mashambulio ya Israel dhidi ya Lebanon yalianza baada ya wanajeshi wake 8 kuuawa na wengine 2 kutekwa nyara na Hezbollah baada ya kuvamiwa kwenye kituo cha mpakani.