Beirut. Hizboullah wakutana na chama cha upinzani nchini Lebanon cha druze.
28 Machi 2005Upande wa upinzani unaoipinga Syria nchini Lebanon umefanya mazungumzo na chama kinachoungwa mkono na syria cha Hizbollah. Baada ya kukutana na kiongozi wa Hizbollah Sheikh Hassan Nasrallah, kiongozi wa upinzani wa chama cha Druze Walid Jumblatt amesema kuwa kundi hilo linaloungwa mkono na Syria litaendelea kuwa na silaha hadi pale Israel itakapoondoka katika maeneo ya mpaka na nchi hiyo. Huo ni mkutano wa kwanza kati ya pande hizo mbili tangu kuuwawa kwa waziri mkuu wa zamani wa Lebanon Rafik Hariri mwezi Februari.
Hizboullah chama pekee cha kisiasa nchini Lebanon kilicho na silaha hadi sasa baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 1975 hadi 1990 na kupambana na majeshi ya Israel kusini mwa Lebanon mwaka 2000.
Wakati huo huo majeshi ya Syria yameondoka katika eneo yalipoweka silaha zake dhidi ya mashambulizi ya angani nchini Lebanon jana. Ikikumbana na mbinyo kutoka jumuiya ya kimataifa pamoja na maandamano ya kuipinga yaliyofanywa na Walebanon, Syria imeahidi kuondoa majeshi yake kabla ya uchaguzi mkuu hapo mwezi wa May.