Beirut. Duru ya pili ya uchaguzi inafanyika nchini Lebanon.
5 Juni 2005Uchaguzi unaendelea katika eneo la kusini ya Lebanon katika duru ya pili kati ya nne za uchaguzi wa bunge kufuatia kuondoka kwa majeshi ya Syria hapo mwezi wa April.
Leo kiasi cha raia 675,000 wanapiga kura. Makundi mawili ambayo yanaiunga mkono Syria, Hizboullah na Amal, ambayo hadi mwaka 2 000 yalikuwa yanapambana na majeshi ya uvamizi ya Israel kusini mwa Lebanon, yanatarajiwa kushinda viti vingi, kati ya viti 23 vinavyogombaniwa katika eneo hilo.
Duru ya kwanza ya uchaguzi iliyofanyika wiki iliyopita katika mji mkuu Beirut mshindi alikuwa Saad Hariri, mtoto wa waziri mkuu wa zamani aliyeuwawa Rafik Hariri, kifo ambacho kilisababisha mzozo dhidi ya Syria hapo Februari mwaka huu.
Jana Jumamosi mjini Beirut mamia ya waombolezaji, ikiwa ni pamoja na mabalozi wa nchi za nje, walihudhuria mazishi ya mwandishi habari ambaye alikuwa akiipinga Syria Samir Kassir.
Aliuwawa kwa bomu lililolipuka katika gari yake siku ya Alhamis. Viongozi wa upande wa upinzani nchini Lebanon wanailaumu Syria kwa mauaji hayo.