Beijing. Waandamanaji washambulia ubalozi wa Japan nchini China.
9 Aprili 2005Katika mji mkuu wa China Beijing, waandamanaji wamevunja madirisha na kutupa mawe katika ubalozi wa Japan pamoja na maeneo mbali mbali ya biashara.
Hii imekuja wakati wa maandamano dhidi ya historia ya wakati wa kivita ya japan na nia yake ya kupata kiti cha kudumu katika baraza la usalama la umoja wa mataifa. Machafuko yalianza wakati maandamano hayo yalipopita katika mgahawa mmoja wa Kijapan. Baadhi ya waandamanaji walitupa chupa na mawe, na kuvunja baadhi ya madirisha ya mgahawa huo.
Waandamanaji pia walishambulia tawi la benki moja ya Tokyo Mitsubishi. Hii inakuja kiasi cha wiki moja baada ya serikali ya China kuishutumu Japan kwa kuidhinisha kitabu cha shule ambacho wakosoaji wanasema kinaondoa makosa yote ya kivita yaliyotendwa na Japan wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia.