1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIJING: Masharti ya Pyongyang kufunga mtambo wa nyuklia

17 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCIB

Korea ya Kaskazini imesema,haitofunga vituo vyake vya nyuklia mpaka Marekani itakapoachilia pesa zote zilizozuiliwa katika benki ya Macau. Mpatanishi mkuu wa Korea ya Kaskazini katika majadiliano ya nyuklia,Kim Kye-gwan alitamka hayo alipowasili mji mkuu wa China,Beijing ambako siku ya Jumatatu majadiliano kati ya nchi sita yataendelea kuhusika na miradi ya nyuklia ya Korea ya Kaskazini.Nchi hizo sita ni China, Urussi,Marekani,Japan na Korea zote mbili.Wakati huo,Kye-gwan akaongezea kuwa wakaguzi wa mitambo ya nyuklia wa Umoja wa Mataifa,hawatoruhusiwa kuingia Korea ya Kaskazini ilimradi kinu cha nyuklia cha Yongbyon kinaendelea kufanya kazi. Kimsingi,Korea ya Kaskazini imekubali kusitisha miradi yake ya nyuklia na badala yake vikwazo vilivyowekwa dhidi ya nchi hiyo viondoshwe.