1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nguli wa kandanda Beckenbauer azungumza kwa mara ya kwanza

27 Oktoba 2015

Nguli wa kandanda wa Ujerumani Franz Beckenbauer amekiri kwa mara ya kwanza kuwa alifanya "kosa" katika mchakato wa kuandaa Kombe la Dunia la FIFA 2006 lakini amekanusha kuwa kura zilinunuliwa

https://p.dw.com/p/1GufJ
Deutschland Franz Beckenbauer
Picha: Reuters/M. Rehle

Beckenbauer alikuwa kiongozi siyo tu wa kamati ya maandalizi ya Kombe la Dunia lakini pia kamati iliyowasilisha ombi la Ujerumani. Siku kumi zilizopita, jarida la Ujerumani, Der Spiegel liliishtumu kamati iliyosimamia ombi la Ujerumani kwa kununua kura.

Beckenbauer mwenye umri wa miaka 70 amesema kamati hiyo ilikubali pendekezo ambalo "lilistahili kukataliwa" na akasema kuwa "aliwajibika kikamilifu kutokana na kosa hilo", isipokuwa ameongeza katika taarifa yake kuwa "hakuna kura zilizonunuliwa".

Kiongozi wa Kandanda la Ujerumani Wolfang Niersbach anaendelea kukabiliwa na maswali zaidi kutoka kwa bodi ya shirikisho la kandanda la Ujerumani – DFB, baada ya matamshi yake ya awali kuhusu malipo ya dimba la Kombe la Dunia la 2006 yaliyotolewa kwa FIFA mnamo mwaka wa 2002, kuacha wazi maswali mengi kuliko majibu yaliyotolewa.

Niersbach anasema hawezi kufafanua kikamilifu kuhusu malipo hayo ya euro milioni 6.7 yaliyotolewa kwa FIFA, mwaka mmoja kabla ya Ujerumani kuandaa Kombe la Dunia 2006.

Kwa mara nyingine alikanusha ripoti iliyochapishwa na gazeti la Der Spiegel kuwa hazina maalum ilitengwa ili kuiwezesha kamati ya maandalizi ya Ujerumani kutoa hongo kwa maafisa wa FIFA ili wawape kibali cha kuandaa tamasha hilo.

Lakini alikiri kuwa kulikuwa na maswali yanayohitaji majibu kuhusiana na malipo hayo, ambayo kamati ya maandalizi ilitoa kwa FIFA mwaka wa 2005. Shirikisho la DFB ambalo linaongozwa na Niersbach, limesema yalikuwa ya mpango wa kiutamaduni wakati wa dimba hilo.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba