Bayern yatumai kugeuza kipigo dhidi ya PSG
12 Aprili 2021Safu ya ulinzi ya PSG ilifanya kazi isioridhisha katika kuizuia Bayern Munich wiki iliyopita, ikiruhusu mashuti 31 dhidi yake. Licha ya kuruhusu mashuti hayo, PSG iliibuka na ushindi wa magoli 3-2 uwanjani Allianz Arena, lakini kutokuwepo kwa mlinzi hodari na nahodha wake Marquinhos katika mechi ya marudiano kesho Jumanne kunaibua hali ya wasiwasi kwa mabingwa hao wa ligi kuu ya Ufaransa.
Raia huyo wa Brazil huenda akaikosa mechi ya kesho kutokana na jeraha. Beki huyo hakufanya mazoezi na kikosi cha PSG leo Jumatatu.
Marquinhos alifunga bao la pili la PSG baada ya kupokea pasi ya staa Neymar japo aliondolewa katika dakika ya 60 ya mchezo na aliikosa mechi ya mwishoni mwa wiki kwa sababu ya jeraha.
Kocha wa PSG Mauricio Pochettino amesema uamuzi wa iwapo Marquinhos atacheza au la katika mechi ya kesho utachukuliwa baadaye. Hata hivyo, iwapo ataikosa mechi hiyo, Pochettino anatarajiwa kuwaanzisha Presnel Kimpembe na Danilo Pereira katika nafasi ya beki wa kati.
"Sote tunazijua sifa za Marquinhos. Yeye ndiye kiongozi wetu katika nafasi ya ulinzi." Kimpembe aliwaambia waandishi wa habari leo Jumatatu. "Yeye ni nahodha wetu. Iwapo hatakuwepo, litakuwa pengo kubwa, lakini kuna wachezaji wengine wenye uwezo wa kujaza nafasi yake."
Habari njema kwa PSG ni kuwa mabingwa watetezi wa ligi ya mabingwa Bayern Munich pia watazikosa huduma za mshambuliaji Robert Lewandowski, Corentin Tolisso na winga Serge Gnabry. Bayern ilitoka sare ya 1-1 na Union Berlin mwishoni mwa wiki katika ligi kuu ya Bundesliga.
Kocha wa Bayern Munich Hansi Flick amesema "Tunataka kugeuza matokeo katika mechi ya marudio mjini Paris. Hakika, tutakuwa na furaha iwapo hilo litatokea."
Chelsea pia inaingia uwanjani Stamford Bridge kesho Jumanne kupambana na FC Porto ya Ureno ilhali siku ya Jumatano, Borussia Dortmund itavaana na Manchester City kabla ya Liverpool kuialika Real Madrid ugani Anfield.