Bayern yatota, Gladbach yapaa, yaiwinda Dortmund
26 Novemba 2018Borussia Moenchengladbach imerejea katika nafasi yake ya pili katika msimamo wa ligi ya Ujerumani Bundesliga jana kwa kuonesha mchezo mwingine mzuri wa kushambulia na kuichapa Hannover kwa mabao 4-1.
Ni viongozi wa ligi hiyo tu Borussia Dortmund ambayo imezisalimia mara nyingi nyavu za adui , ikiwa imeweka wavuni mabao 35 katika michezo 12 ya ligi msimu huu, wakati Gladbach imefikisha mabao 30 licha ya kuanza mpambano wa jana kwa kuwa nyuma kwa bao moja katika sekunde ya 12 tangu mchezo huo kuanza.
Mshambuliaji kutoka Marekani Bobby Wood aliweka wavuni bao safi sekunde chache baada ya kuanza mchezo kwa Hannover na kutimiza bao lake la tatu msimu huu. Wakati huo hakuna mchezaji wa Gladbach aliyeugusa mpira.
Mchezo huo hata hivyo uliingia dosari baada ya mlinzi wa Gladbach Matthias Ginter kugongana na Noah Joel Sarenren Bazee wa Hannover. Baada ya kupatiwa matibabu uwanjani Ginter aliondolewa uwanjani hapo kwa machela na kupelekwa hospitali. Taarifa zinasema kuwa mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Ujerumani pia hataweza tena kucheza katika mwaka huu wa 2018 . Mchezaji huyo ameumia katika sehemu ya jicho lake pamoja na mfupa wa shavu.
Bayern yatumbukia katika matatizo
Werder Bremen imefikisha mwisho mfululizo wa michezo mitatu bila ushindi kwa kutoka sare ya bao 1-1 jana Jumapili dhidi ya Freiburg. Hata hivyo Bremen inabakia katika nafasi ya saba katika msimamo wa ligi ya Ujerumani.
Bayern Munich imetumbikia katika hali ngumu msimu huu baada ya kutopata matokeo mazuri katika ligi kwa zaidi ya michezo minne, na iko nyuma ya Borussia Dortmund inayoongoza ligi hiyo kwa pointi tisa. Bila shaka hili si jambo la kawaida kwa vigogo hao wa soka nchini Ujerumani, lakini baada ya kutoka sare ya mabao 3-3 dhidi ya timu iliyopanda daraja msimu huu Fortuna Dusseldorf nyumbani katika uwanja wa Alianz Arena, hali si shwari tena.
Kocha Nico Kovac anasema ameumia sana kwa matokeo hayo:
"Mnaweza kufikiria vile ninavyojisikia. Sifahamu iwapo hasira zinazidi kupanda , kwasababu , wakati mchezo umekwisha udhibiti na katika dakika za mwisho bao linarejeshwa. Kwanza tuliongoza kwa mabao 2-0 na kabla ya mapumziko matokeo yanakuwa 2-1. Tuliongoza tena kwa mabao 3-1 na kisha katika dakika ya 92 inakuwa 3-3. Siwezi kuwa na furaha, na nimekasirika sana na naelewa kuhusu uwezo wetu wa kujilinda ambao hatukuweza kuutumia, kibaya zaidi ni jinsi tulivyojilinda wakati tunafungwa bao la tatu."
Honnes amkingia kifua Kovac
Hata hivyo kocha wa Furtuna Dusseldorf Friedel Funkel amesema amefarijika sana kuona timu yake ilivyopambana katika uwanja wa ugenini mjini Munich na kupata sare hiyo.
"Bila shaka nimefurahi sana kwamba kabla ya firimbi ya mwisho ya mchezo tuliweza kupachika bao la kusawazisha. Na hii ikiwa baada ya kuwa nyuma kwa mabao mawili, lakini hatukupoteza mwelekeo wetu. Tuliendelea kulinda lango letu kwa pamoja. Na iwapo Bayern wangepata bao la 4 kila kitu kingekuwa kimemalizika. Na tulikuwa tu na matumaini kwamba hali itakwenda vizuri kwetu, na tungeweza kufanya vizuri kwa kutumia kasi ya mshambuliaji wetu Dodi Lukebakio."
Mjadala mkali unaendelea hivi sasa kuhusu kocha Nico Kovac, kutokana na matokeo hayo mabaya kwa Bayern Munich. Kuna majina kadhaa yanayotajwa , lakini vyombo vya habari za michezo nchini Ujerumani zinajaribu kuibua minong'ono ya majina kama Arsene Wenger kocha wa zamani wa Arsenal London.
Huyu anafikiriwa huenda akachukua nafasi ya Nico Kovac kwa kuwa Bayern inahitaji kocha mwenye jina kubwa katika medani ya soka, na pia mwenye uzoefu. Piam kuna jina la Ralph Hasenhuetel , aliyekuwa kocha wa zamani wa RB Leipzig ya Ujerumani na pia Mark van Bommel kocha wa sasa wa PSV Eidhoven. hata hivyo rais wa Bayern Munich Uli Honness anamkingia kifua Nico Kovac kwa kusema.
"Timu ilicheza kwa tahadhari sana katika kipindi cha kwanza na pia kwa upande wa kasi, hatujacheza kama ilivyotarajiwa. Lakini kipindi cha pili timu ilianza kujiamini zaidi na nadhani katika kipindi cha pili timu ilicheza vizuri zaidi."
Eintracht Frankfurt imechupa hadi nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi, kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Augsburg , wakati RB Leipzig iliyoko katika nafasi ya nne ilikwaa kisiki dhidi ya Wolfsburg kwa kukubali kipigo cha bao 1-0.
Bayern iko nafasi ya nne ikifuatiwa na TSG Hoffenheim iliyotoka sare na Hertha Berlin ya mabao 3-3. Fortun a Dusseldorf licha ya kutoka sare na bayern Munich inashikilia nafasi ya 17 ikiwa na pointi 9, ikiwa katika nafasi ya kushuka daraja.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe /rtre / ape / dpae
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman