Bayern yairarua Frankfurt katika Super Cup
13 Agosti 2018
Robert Lewandowski alipachika wavuni mabao matatu wakati Bayern Munich ikinyakua kombe la Super Cup la Ujerumani jana Jumapili kwa kuirarua Eintracht Frankfurt kwa mabao 5-0 katika mwanzo mzuri kwa kocha Niko Kovac , ambaye msimu uliopita alikuwa akiifunza timu hiyo ya frankfurt na kunyakua kombe la DFB Pokal kwa kuishinda Bayern kwa mabao 3-1 mjini Berlin mwishoni mwa msimu uliopita. Mshambuliaji huyo kutoka Poland , ambaye hakufanya vizuri katika fainali za kombe la dunia , 2018, alizima purukushani za timu ya zamani ya Kovac kwa kupachika mabao mawili katika muda wa dakika tano katika kipindi cha kwanza.
Ligi ya England Premier League imeanza rasmi mwishoni mwa wiki hii na timu zilizomaliza katika nafasi tano za juu zimepata ushindi bila taabu, ambapo mabingwa watetezi Manchester City iliichapa Arsenal London kwa mabao 2-0 jana Jumapili. Hata hivyo kocha wa Arsenal Unai Emery amesema timu yake inahitaji kukubaliana zaidi na mbinu zake lakini ameeleza pia kwamba kuna ishara nzuri alizoona katika mchezo huo wa ufunguzi licha ya kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Manchester City.
Kocha wa Manchester City Pep Guardiola anataka Raheem Sterling kuitumikia timu hiyo kwa muda mrefu zaidi baada ya mshambuliaji huyo kuonekana kuchukua jukumu kubwa la kuiongoza timu hiyo katika ushindi wa mchezo wa ufunguzi katika Premier League dhidi ya Arsenal. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 ambaye amebakiza miaka miwili katika mkataba wake , alipachika bao lake la 50 la ligi jana Jumapili wakati mabingwa hao watetezi wakianza kampeni ya msimu mpya kwa ushindi wa mabao 2-0 ugenini.
"Tunafurahia kile anachokifanya na tungependa abakie, Guardiola aliwaambia waandishi habari. Vyombo vya habari vya Uingereza vimeripoti kwamba wasimamizi wa Sterling wanataka mkataba mpya ambao atalipwa pauni 300,000 kwa wiki , ambao utanfanya kuwa mchezaji anayelipwa fedha nyingi katika klabu hiyo.
Paris St. Germain imeanza msimu mpya jana kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Caen, kwa magoli ya Neymar, Adrien Rabiot na Tomothy Weah. Kocha mpya wa PSG Thomas Tuchel aliwaweka nje Kylian Mbappe, Edson Cavani na Marco Verratti wakati akianza msimu wake wa kwanza na klabu hiyo maarufu ya Uufaransa na kuwatumia chipukizi Colin Dagba, Stanley N'Soki na Antoine Bernede. PSG ilimaliza mchezo huo ikiwa na wachezaji sita waliochini ya umri wa miaka 20.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / dpae / afpe
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman