Bayern wapepea, wapinzani wabaki hoi
10 Desemba 2012Hii ni baada ya mabingwa hao watetezi wa Bundesliga, kuathirika na makosa ya refarii ambayo yaliwanyima ushindi katika mchuano wa nyumbani Jumamosi dhidi ya Wolfsburg. Bayern waliendeleza kampeni yao kwa kusajili ushindi wa magoli mawili kwa sifuri dhidi ya watani wao Augsburg. Nao Borussia Dortmund wakashindwa na Wolfsburg magoli matatu kwa mawili. Refa Wolfgang Stark ameomba radhi kwa kufanya maamuzi ambayo hayakuwa sahihi.
Kwanza alipeana mkwaju wa penalti dhidi ya Dortmund na kumtimua uwanjani beki wao Marcel Schmelzer. Stark amesema ameangalia video ya mchezo na anakiri kufanya makosa. Ameomba radhi akisema hilo halitatokea tena. Schmelzer alionekana kuunawa mpira lakini video zilionyesha mpira uligonga goti lake ijapokuwa uligusa kidogo ngume, na wala mchezaji huyo hakuunawa mpira. Bayer Leverkusen nao waliduwazwa nyumbani baada ya Hanover kuwazaba magoli matatu kwa mawili na sasa wako katika nafasi ya pili nyuma ya Bayern na tofauti ya pointi 11. Borussia Moenchengladbach wapata ushindi wa magoli mawili kwa sifuri nyumbani dhidi ya Mainz. Eintracht Frankfurt walifunga magoli mawili katika dakika moja na kupata ushindi wa magoli manne kwa moja nyumbani dhidi ya Werder Bremen. Schalke walishindwa kutamba baada ya kushindwa manbao matatu kwa moja dhidi ya VfB Stuttgart.
United yaongoza katika Premier League - Uingereza
Kule Uingereza, Manchester United wamesonga mbele kileleni na tofauti ya pointi sita baada ya kuwashinda watani wao Manchester City magoli matatu kwa mawili uwanjani Etihad jana, huku Robin van Persie akifunga bao la ushindi katika dakika za majeruhi. United sasa wana pointi 39 kutokana na mechi 16 mbele ya City ambao wana 33. Fernando Torres aliifungia Chelsea magoli mawili katika ushindi wa tatu moja dhidi ya Sunderland. Chelsea wako katika nafasi ya tatu na pointi 29 wakati wakishiriki katika dimba la Kombe la Vilabu nchini Japan. Everton ni wan ne na pointi 26 baada ya kuwapiku Tottenham magoli mawili kwa moja.
Nchini Italia katika Serie A, Juventus wanaongoza na pointi 38, pointi nne mbele ya Inter Milan ambao wako katika nafasi ya pili. Juve waliwalaza Palermo goli moja kwa sifuri wakati Inter ikiinyamazisha Napoli magoli mawili kwa moja.
Messi avunja rekodi
Bila shaka habari zinazogonga vichwea vya habari siyo Uhispania tu bali kote ulimwenguni ni umahiri wa mshambuliaji Lionel Messi, ambaye amevunja rekodi ya kufunga magoli mengi katika kipindi cha mwaka mmoja. Messi mwenye umri wa miaka 25, amefunga jumla ya magoli 86 baada ya kufunga goli lake la pili jana katika mchuano wa La Liga Uhispania nyumbani kwa Real Betis, na kuipiku rekodi iliyowekwa na Gerd Mueller miaka 40 iliyopita ya magoli 85. Mchezaji huyo anayepigiwa upatu kutwaa tena kwa mara ya nne mfululizo tuzo ya mchezaji bora wa mwaka mwezi ujao, ameifungia Barca magoli 74 na 12 Argentina katika mwaka wa 2012 na kuivunja rekodi ya Mueller ya Bayern Munich na Ujerumani mwaka wa 1972. Ametikisa wavu mara 56 katika La Liga, 13 katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, mara tatu katika kombe la Mfalme na mara mbili katika kombe la Super Cup la Uhispania nab ado kuna mechi mbili za La Liga, na mechi moja ya Kombe la Mfalme kuongeza kwa idadi yake kabla ya kumalizika mwaka huu.
Manny Pacquiao azidiwa nguvu na Marquez
Katika ndondi shujaa wa ndondi wa Ufilipino Manny Pacquiao ametiririkwa na machozi kwenye televisheni ya taifa akisema ameifedhehesha nchi baada ya kurambishwa sakafuni kwa njia ya knock out na hasimu wake kutoka Mexico Juan Manuel Marquez. Pacquiao amekiri kushindwa, akisema hiyo ni kazi yake, lakini ana machungu kuona jinsi Ufilipino ilivyohuzunika kutokana na kichapo hicho. Tukisalia na mambo ya ndondi, ni kwamba suali kubwa linalosalia kuulizwa na mashabiki katika mwaka wa 2013, ni Nani anayeweza kuwasimamisha ndugu wawili Klitschko katika kitengo cha uzani wa heavyweight? Kwa sasa hakuonekani mpinzani anayeweza kufanya hivyo.
Baada ya kushikilia mataji ya WBA, IBF, IBO na WBO kwa miezoi 18 iliyopita, Wladmir Klitschko alipata ushindi wake wa 69 katika taaluma yake mnamo mwezi Novemba wakati alipopata ushindi kupitia wingi wa pointi dhidi ya Mariusz Wach wa Poland. Kama kawaida kulikuwa na uvumi kuhusu pigani baina ya pengine Witali, bingwa wa WBC au Wladmir dhidi ya David Haye wa Uingeerza, ambaye alirudi tena ulingoni baada ya kustaafu na kumrambisha sakafuni kwa njia ya knock put David Chisora mwezi Julai.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Josephat Charo