1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern Munich yaendelea kutamba

24 Novemba 2014

Bayern Munich na Chelsea zimeendelea kutamba katika ligi za Bundesliga na Premier league, wakati mshambuliaji wa Barcelona Lionel Messi aweka rekodi mpya ya kufunga mabao katika La Liga.

https://p.dw.com/p/1DsIj
Fußball Bundesliga FC Bayern München vs. TSG 1899 Hoffenheim
Bayern Munich wakipiga bao dhidi ya HoffenheimPicha: Reuters/M. Dalder

Mabingwa watetezi wa ligi ya Ujerumani Bundesliga , na viongozi wa sasa wa ligi hiyo Bayern Munich imepanua uongozi wao hadi ponti saba baada ya kuirarua Hoffenheim kwa mabao 4-0 wakati Bastian Schweinsteiger akicheza kwa mara ya kwanza tangu kupata maumivu katika fainali za kombe la dunia nchini Brazil.

Mshambuliaji wa Bayern Arjen Robben amemwagia sifa mchezaji huyo wa kati kwa kusema mfalme wa soka amerejea dimbani.

"Mfalme wa soka amerejea. Ilikuwa ni muda mrefu. Bastian Schweinsteiger amekuwa na matatizo mengi na tunapaswa sasa kumsaidia. Ni mwanzo tu, lakini kama ukimwangalia, inafurahisha, wakati akiingia tu na kufanya alivyofanya. Amefanya vizuri sana."

Fußball Bundesliga Borussia Dortmund vs. SC Paderborn 07
Wachezaji wa Borussia Dortmund wakishangiria baoPicha: Reuters/I. Fassbender

Mabingwa hao kutoka Bavaria wameweka rekodi ya klabu yao kwa kufungwa mabao 3 tu katika michezo 12 ya ligi na hawajafungwa katika mashindano yote ya msimu huu. VFL Wolsburg imeendelea kushikilia nafasi ya pili licha ya kufungwa na Schalke 04 siku ya Jumamosi.

Makamu bingwa wa msimu uliopita Borussia Dortmund imeendelea na hali ya kusua sua , ikipoteza uongozi wa mabao 2-0 katika kipindi cha kwanza na kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Paderborn iliyopanda daraja msimu huu na pia kupata pigo la kumpoteza mchezaji wake muhimu Marco Reus ambaye hataonekana tena uwanjani hadi mapema mwakani.

Wakati huo huo kocha wa VFB Stuttgart Armin Veh amejiuzulu leo Jumatatu , siku moja baada ya kikosi chake kupoteza mchezo nyumbani kwa bao 1-0 dhidi ya Augsburg na inabakia mkiani mwa ligi ya bundesliga.

mchezaji wa Augsburg Marvin Hitz amesema.

"Nafikiri leo tumecheza vizuri sana. Kwa kuwa na wachezaji wengi zaidi uwanjani ni dhahiri ilikuwa rahisi kwetu kuutawala mchezo, lakini pamoja na hayo tuliweza tu kupata nafasi mbili za wazi, ambapo mlinda mlango alifanyakazi nzuri. Na kisha tulipata bao la mkwaju wa penalti, huenda ni kwa bahati, sijaweza kuona vizuri na pamoja na hayo tunafurahi kupata ushindi huu."

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / ape / rtre
Mhariri: Mohammed Khelef