Bayern Munich kidedea dhidi ya Dortmund
7 Agosti 2017Bayern Munich siku ya Jumamosi ilitoka kidedea katika uwanja wa Signal Iduna Park mjini Dortmund baada ya kuishinda Bourissia Dortmund kwa mabao 7-6 kwa njia ya mikwaju ya penalti baada ya timu hizo vigogo katika ligi ya Ujerumani Bundesliga kutoshana nguvu katika dakika 90 za kawaida kwa kufungana mabao 2-2. Hata hivyo kulikuwa na kwikwi katika mchezo huo kutokana na kushindwa kufanyakazi mfumo wa kutambua mabao kwa njia ya vidio ikiwa ni jaribio la kwanza kubwa kabla ya kutumika mfumo huo katika ligi ya Bundesliga.
Chama cha kandanda nchini Ujerumani DFB na chama kinachoendesha ligi hiyo DFL, vimesema katika taarifa ya pamoja kwamba mfumo huo wa kuwasaidia waamuzi kwa njia ya video ulishindwa kufanyakazi katika mchezo huo wa Jumamosi nyumbani kwa Borussia Dortmund, na kuzusha mjadala juu teknolojia hiyo mpya.
Refa alikuwa ana jaribu kutambua iwapo Joshua Kimmich wa Bayern Munich alikuwa ameotea wakati alipompatia pasi Robert Lewandowski na kupachika bao la kusawazisha bao la Dortmund lililowekwa kimiani na Christian Pulisic katika dakika za mwanzo.
Mistari ya kuonesha kwamba mchezaji ameotea ama la katika video haikuwapo katika sehemu ya kwanza ya mchezo huo kutokana na matatizo ya kiufundi, wamesema maafisa wa vyama hivyo , ikiwa na maana refa alilazimika kutoa uamuzi bila ya mfumo huo wa usaidizi.
Ligi ya Ujerumani inaanza rasmi tarehe 18 mwezi huu, siku ya Ijumaa kwa mchezo kati ya mabingwa watetezi Bayern Munich dhidi ya Bayer Leverkusen.
Dortmund inaanza kampeni ya msimu huu ugenini dhidi ya Wolfsburg , siku moja baada ya ufunguzi wa msimu , na wanakabiliwa na mwanzo mgumu kwa kupambana na Hertha Berlin , kisha Freiburg na FC Kolon , timu zote zikiwa katika timu saba bora za ligi msimu uliopita.
Mwandishi: Sekione Kitojo/dpae,afpe,rtre,ape
Mhariri: Mohammed Khelef