Bayer Leverkusen yamtimua kocha Robin Dutt
2 Aprili 2012Dutt alifika mbele ya Mkurugenzi wa Spoti wa Leverkusen Rudi Voeller na Mwenyekiti Wolgang Holzhaeser Jana Jumapili asubuhi ambapo alipigwa kalamu rasmi. Katika kipindi kilichosalia cha msimu na michuano sita ijayo, beki wa zamani wa Leverkusen na Liverpool raia wa Finland Hyypia atakuwa kocha pamoja na mkufunzi wa kikosi cha Leverkusen cha wachezaji wasiozidi umri wa miaka 19.
Bayer ni mojawapo ya timu nne ambazo zina pointi 40 na ni sharti zimalize miongoni mwa timu saba za kwanza ili kujihakikishia nafasi ya kucheza katika Europa League, baada ya timu hiyo kufikia awamu ya 16 ya ligi ya Mabingwa Ulaya. Dutt ni kocha wa nane kufurushwa na klabu ya Bundesliga msimu huu.
Anafuata Marcus Sorg (Freiburg), Michael Oenning (Hamburg), Holger Stanislawski (Hoffenheim) na Marco Kurz (Kaiserslautern), huku nayo Hertha Berlin ikawapiga kalamu Markus Babbel na kisha Michael Skibbe msimu huu.
Vita vya taji la Bundesliga vyashika kasi
Bayern Munich walipunguza uongozi wa Borussia Dortmund hadi tofauti ya alama tatu baada ya miamba hao wa Ujerumani kuwashinda mahasimu wao Nuremberg goli moja kwa sifuri.
Mabingwa Dortmund walitekwa sare ya magoli manne kwa manne nyumbani na Stuttgart Ijumaa usiku, na nambari mbili Bayern wakaitumia vyema fursa hiyo ambapo Mholanzi Arjen Robben alijitwika jukumu la kufunga bao.
Hannover waliendeleza rekodi yao ya kutoshindwa nyumbani na kusonga hadi nafasi ya tano baada ya kusajili ushindi wa mabao mawili kwa moja dhidi ya Borussia Moenchengladbach. Didier Ya Konan alifunga goli la kwanza naye Mame Biram Diouf akamaliza kazi. Schalke 04 nao walikua na wakati mgumu dhidi ya Hoffenheim lakini walimudu tu sare ya goli moja.
Katika habari nyingine za Bundesliga ni kuwa mshambuliaji wa Bayern Munich Arjen Robben anakaribia kuurefusha mkataba wake na mabingwa hao mara nne wa Ulaya. Hayo yamesemwa na Kocha Jupp Heynckes. Mholanzi huyo Robben alijiunga na Bayern mnamo mwaka 2009 akitokea Real Madrid na mkataba wake unakamilika mwaka 2013.
Nani atafuzu nusu fainali Ligi ya Mbaingwa Ulaya?
Mechi za marudiano za robo fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya UEFA Champions League zinarejea Jumanne. Pambano baina ya miamba ya soka Ulaya Barcelona na AC Milan ndilo linaloonekana kuwa la wazi zaidi wiki hii wakati Real Madrid na Bayern Munich tayari wana mguu mmoja ndani ya nusu fainali nao Chelsea wanaonekana kuwa katika hali nzuri.
Mabingwa watetezi Barcelona walitoka sare ya bila kufungana na AC Milan wiki iliyopita na vijana hao wa Pep Guardiola wanapigiwa upatu kufuzu kesho katika nusu fainali.
Pia Jumanne klabu ya Bayern Munich itafunga kazi dhidi ya Olympique Marseille nyumbani Allianz Arena. Bayern ambao wanalenga kufika fainali ya kombe hilo ambayo itachezwa katika uwanja wao wa nyumbani, watakuwa bila kiungo Bastian Schwinsteiger ambaye anatumikia adhabu y akadi ya njano, aliyopata kule Marseille.
Wachezaji sita wa Bayern wakiwemo Thomas Muller, nahodha Philip Lahm, Toni Kroos na David Alaba wanafahamu kuwa kadi ya njano kwao inaweza kuwanyima fursa ya kucheza mchuano wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali dhidi ya Real Madrid ambao tayari waliwafunga APOEL Nicosia ya Cyprus magoli matatu kwa sifuri na watakutana Jumatano katika uga wa Santiago Bernabeu.
Chelsea ambao wana faida ya goli moja kwa sifuri watacheza nyumbani dhidi ya Benfica Jumatano na kuimarika kwa klabu hiyo ya London chini ya kaimu mkufunzi Roberto Di Matteo, naye Fernando Torres akionekana kuimarika inamaanisha klabu hiyo inafaa kufuzu. Mhispania huyo anatarajiwa kuhifadhi nafasi yake kwa vile Didier Drogba ana tatizo la mguu. Beki wa zamani wa Benfica David Luiz pia anataliwa shaka.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters/AFP
Mhariri: Yusuf, Saumu