1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barua kutoka Dar: Vyama vya upinzani Tanzania ndo vinapotea?

Anaclet Rwegayura16 Novemba 2020

Bunge la 12 la Tanzania tayari limezinduliwa rasmi huku likiwa na wabunge wengi wa CCM. Je hilo ndo anguko la vyama vya upinzani Tanzania? Ni swali linalojibiwa na Anaclet Rwegayura katika makala ya Barua kutoka Dar.

https://p.dw.com/p/3lMlf
Tansania Amtseid des Präsidenten John Pombe Magufuli
Picha: Tanzania Presidential Press Service

Vyama vya upinzani vimeshindwa mfululizo katika chaguzi sita za urais kila miaka mitano na mwaka huu vimepigwa chini kwa kishindo. Kulingana na Rais Magufuli, maendeleo ya kitaifa hayana rangi ya kisiasa. Lakini Watanzania wanajiuliza kwa nini vyama vya upinzani vimeshindwa vibaya katika ngazi zote za uchaguzi mkuu wakati huu.

Je, wagombea wao waliungwa mkono na walaghai ambao hata hawakujitokeza kupiga kura Siku ya Uchaguzi? Je, wagombea wao walishindwa wakati wa  kampeni kuwadhihirishia wafuasi wao kuwa wangekuwa wawakilishi wa kuaminika? Kwa jumla, sura na sauti ya vyama hivi imepotea na hivyo hivyo hata ushawishi wao kwa umma.

Tansania Opposition Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa chadema Freeman MbowePicha: Ericky Boniphace/AFP/Getty Images

Wakati Tanzania ilipoanza kujaribu mfumo wake wa vyama vingi baada ya miongo kadhaa ya utawala wa chama kimoja, ambacho wachambuzi waliona kama hakiridhishi kutokana na ufisadi na urasimu, umma kwa jumla ulikubali mabadiliko hayo kama hatua ya kwanza katika mwelekeo sahihi.

Mwelekeo huo ulipanua mazingira ya kisiasa ambayo yaliwapa watu uhuru zaidi na njia ambazo wangeweza kutolea maoni yao au kukosoa chochote kilichofanyika kinyume na masilahi yao. Hadi sasa sehemu kubwa ya watu bado inahitaji kuletwa katika mfumo jumuishi kisiasa ili watoe maoni kuhusu wanavyoshiriki katika maendeleo ya nchi.

Wabunge wameapishwa na sehemu ya vyama vya upinzani ikiwa na idadi ndogo kabisa jambo ambalo halikuwahi kutokea katika Bunge hilo la vyama vingi. Je, ushindi mkubwa wa mwaka huu wa CCM ni dalili ya uwezekano wa kutoweka kwa upinzani rasmi katika siasa za Tanzania? Je, mwenendo wa mijadala Bungeni utakuwa vipi ambapo kila mbunge ataunga mkono msimamo wa serikali, labda bila swali?

Spika Job Ndugai amejaribu kuhakikishia umma kwamba halitakuwa Bunge linalosema ama 'Ndio' au "Hapana" kwa kila suala linalowasilishwa kwa majadiliano. Hii inamaanisha wabunge hawatapitisha au kukataa muswada bila kupima faida na hasara zake.
Vyama vya upinzani vinapaswa kujilaumu kwa kushindwa kutambua alama za mabadiliko katika mazingira ya kisiasa, na kujifunza kuboresha mikakati yao baada ya uchaguzi wa 2015. Wakati huo Magufuli alichukua hatamu za nchi kwa falsafa ya 'Hapa kazi tu'. Alisema malumbano ya uchaguzi yalikuwa yameisha na watu wote wafanye kazi kwa bidii.

Sasa ni wakati wao kuchukua hatua na kuona ikiwa wanaweza kufikia kile walichokosa hapo awali. Haitakuwa rahisi na sidhani kama walikuwa wamefanya maandalizi yoyote kwa matokeo ya kimbunga hiki.Magufuli: Uchaguzi umekwisha, kazi sasa ni kudumisha amani

Tansania Dar es Salaam | ACT Wazalendo Vorsitzender - Maalim Seif Sharif Hamad
Aliyekuwa mgombea wa urais Zanzibar kupitia ACT-Wazalendo Maalim Seif Sharif HamadPicha: Ericky Boniphace/DW

Lazima wakabiliane na changamoto kubwa ya kujipanga upya ikiwa wanataka kuonekana wanafanya jaribio fulani mnamo 2025. Wanaweza kuwa na kazi ya ziada kabla ya uchaguzi ujao. Ninazungumza juu ya kuleta mvuto mzuri kwa staili mpya kabisa ya kuwafikia wapiga kura ambao tayari wamekuwa kando na ahadi zisizotekelezeka.

Wakati huo huo, timu ya CCM inafanya kazi usiku kucha kulinda rekodi yake ya kutoshindwa. "Wakati vyama vingine vinasubiri kuiga kile tunachofanya katika CCM, viongozi wetu wa ngazi ya juu wanatafakari hali ya uongozi ambao nchi yetu inapaswa kuwa nayo kesho," alisema mwanaharakati wa chama hicho.

Hakika, siku zijazo zinakaribia kwa kasi ya umeme na huo inapasa uwe mwelekeo wa kila chama na mabadiliko katika fikra. Mabadiliko hayaepukiki na viongozi ambao wanajifanya kupuuza ukweli huu inawezekana baadaye wakajikuta wako tu kama vivutio vya jumba la makumbusho ya kisiasa, kwa sababu ukosefu wa mabadiliko katika maisha ni ishara ya kutoweka.