1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barua kutoka Dar: AU yashindwa kumaliza vita

Admin.WagnerD30 Novemba 2020

Kwa nini Afrika daima huandamwa na nyakati zenye changamoto? Watu wake wanajitahidi kila mwaka kujiunga na fursa za biashara katika masoko kote ulimwenguni, ambapo serikali zao zinakimbizana na kivuli cha amani.

https://p.dw.com/p/3m23w
Tigray-Konflikt | Militär Äthiopien
Picha: Ethiopian News Agency/AP/picture alliance

Wajasiriamali wanajitahidi kufanya maendeleo katika uzalishaji, kuingiza bidhaa sokoni kwa viwango vinavotakiwa na kwa usajili kulingana na kanuni zilizopo, lakini wakat huo huo wahalifu waliokubuhu, mithili ya wadudu waharibu wa mazao shambani, hawajali lolote kuvuruga juhudi hizi.

Serikali zetu zinajitahidi kurekebisha mikataba na wabia wa kimkakati karibu pande zote muhimu kwa ustawi na maendeleo ya taifa, lakini pingamizi hujitokeza nyuma yao kila wakati.

Wakuu wa Nchi na Serikali waliahidi kunyamazisha bunduki na kumaliza vita vyote barani Afrika mwaka 2020. Tunachoona sasa ni uchungu na kushindwa kunakokatisha tamaa. Juhudi zao zimenasa kati ya risasi zinazopishana katika mapigano yasiyokoma kama yanavyoshuhudiwa kila upande wa bara hili.

Äthiopien Konflikt in Tigray | Flüchtlinge in Sudan
Mzozo wa Tigray unasababisha idadi kubwa ya wakimbiziPicha: Ashraf Shazly/AFP/Getty Images

Maelfu ya watu wako mbioni kutafuta hifadhi salama kwa ajili ya maishayao. Hapa tujiulize:. Je, ni Kweli maamuzi na maazimio ya Afrika hutokana na nia ya kweli kujenga amani endelevu? Migogoro ya kivita sasa inaongeza mzigo wa athari za maradhi ya COVID-19 na shinikizo nyingine kwa afya na tija ya mamilioni ya wakazi wa vijijini na mijini.

Februari 2017 niliandika katika safu hii kwamba muda uliowekwa kunyamazisha bunduki haukuzingatia hali halisi barani Afrika, lakini hakuna aliyeonesha  wasiwasi. Ujumbe wangu labda ulionekana haukubaliki kisiasa. Lakini ukweli unabaki kuwa ukweli haijalishi unatamkwa na bingwa wa mambo ya serikali,  mwanasiasa au mwandishi.

Bunduki zimenyamazishwa katika mkoa wa Casamance kusini mwa Senegal ambapo waliotaka kujitenga walipigana vita visivyo na maana kwa miaka mingi, lakini harufu ya risasi bado inazagaa angani katika eneo jirani la Sahel. Waathiriwa wa milipuko ya bunduki wanalazimika kukimbia nchini Mali, Burkina Faso, Jamhuri ya Afrika ya Kati na zaidi mpaka kaskazini mashariki mwa Nigeria ambapo vurugu zisizokoma, kulingana na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, zimechochea mawimbi mapya ya wakimbizi kwenda kwenye kambi zenye msongamano mkubwa mnamo 2020.

Mali Kati PK Putsch Anführer Ismael Wague
Mali imeshuhudia mapinduzi ya kijeshi 2020Picha: Getty Images/AFP/A. Risemberg

Ni hadithi hiyo hiyo tunaipata mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.  Sudan Kusini, Ethiopia, Somalia na Msumbiji ambako watu wanaokimbia makazi yao ni wengi kiasi kwamba Afrika haiwezi kupata ndoto za utulivu. Mipango kadhaa imetangazwa kutoka mji mkuu wa kisiasa wa Afrika, Addis Ababa nchini Ethiopia, juu ya kukomesha mtiririko  wa silaha haramu barani, lakini kushindwa kwa hatua hizi kunaoneshwa kwa aibu na mauaji ya watu wasio na hatia na mateso ya watu katika maeneo ya vita ikiwa ni pamoja na nchi zinazodai kuwa tulivu.

Wakati pazia linashuka kwa mwaka 2020, 'Kunyamazisha Bunduki' inabaki kuwa tangazo la kutamani na lisilo na uhakika la Umoja wa Afrika (AU) ambalo limekosa kuweka alama ardhini. Je, tunahitaji kujenga ngome na tuta au kubuni njia bora zaidi za kuwalinda walio hatarini zaidi ambako bunduki haziwezi kudhibitiwa?

Afrika dhahiri inahitaji kupambana na bunduki na silaha ndogo ndogo kwa kutumia taaluma kama vile baadhi ya nchi zetu zinavyofanya kudhibiti biashara ya dawa za kulevya ili kuondoa janga hili. Bara halitafanikiwa kudhibiti silaha kwa kupitisha maazimio yenye maneno mazito na nyimbo za kaulimbiu bila kuchukua hatua stahiki.

Sudan | Militärregierung PK Putschversuch  vereitelt
Baraza tawala la kijeshi SudanPicha: picture-alliance/AA

Milango inayofunguka pande zote ya Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika (AfCFTA) itakuwa wazi hivi karibuni, lakini nchi wanachama zinajiandaa vipi kudhibiti silaha zisipitie njia hii ya kuratibu ushirikiano huu kwa manufaa ya raia wote?
Biashara huria itakuwa ufunguo wa kumaliza umasikini barani Afrika ikiwa bunduki zitanyamazishwa kabisa. Mambo mengi ambayo watu wengine huyachukulia kuwa ya muhimu kwa maisha mazuri na yenye mafanikio hayafikiriwi au hayapo katika maeneo yanayodhibitiwa na wababe wa vita.

Majambazi hawa hawatoi usafiri wa umma wala kuweka maduka ya bidhaa kama simu za mkononi, seti za runinga, vipodozi na kompyuta mpakato – kwa kutaja machache tu.

Nchi za Kiafrika inabidi zifungue Mwaka Mpya kwa mawazo yao yatokayo nyumbani ili kukabiliana na changamoto kubwa za usalama, janga la Corona, athari za mabadiliko ya hali ya hewa, kufufua uchumi, na biashara - badala ya kusubiri mipango ya utekelezaji iliyowekwa na ofisi za kigeni za wabia wa maendeleo . Tunahitaji kuzungumzia hadithi mpya ya Kiafrika.

Anaclet Rwegayura, Dar es Salaam