Baridi kali yaua zaidi ya watu 160 Ulaya
6 Februari 2012Vijiji vyote vilivyopo katika eneo la mashariki ya Ulaya vilipoteza mawasiliano hapo jana kutokana na baridi kali na theluji, huku maelfu ya wakaazi wake wakishindwa kutoka nje ya nyumba zao.
Hali ya hewa hiyo ambayo haijashuhudiwa kwa miongo kadhaa sasa barani Ulaya, ilisababisha pia barabara kutopitika, usafiri wa ndege na reli kushindwa kufanya kazi na matumizi ya gesi kupanda ghafla katika eneo hilo.
Na wakati watabiri wa hali ya hewa wakionya kutokea kwa baridi kali zaidi siku za usoni, maelfu ya watu nchini Ukraine wanatafuta hifadhi ili kuepukana na theluji hiyo iliyokwishaua jumla ya watu 101, mpaka kufikia leo asubuhi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya kutoka mjini Kiev, takriban watu 1,600 wameomba uangalizi wa kitabibu baada ya kupatwa na homa kali inayoathiri mfumo wa upumuaji na wengine kupata ganzi miguuni kutokana na baridi hiyo kali iliyofikia kiwango cha nyuzi za celisiasi 35 chini ya sifuri.
Na huko mjini Warsaw, Poland watu tisa wamethibitishwa kupoteza maisha baada ya kemikali aina ya zebaki kushuka mpaka kufikia nyuzi za selisiasi 32 chini ya sifuri ambayo ni sawa na nyuzi joto za Fahrenheit 25.6 chini ya sifuri.
Idadi hiyo mpya inaongeza vifo vilivyosababishwa na baridi nchini Poland kufikia watu 29, tangu juma lililopita.
Na mjini London, Uingereza Ofisi inayoshughulikia utabiri wa hali ya hewa imetangaza hali hiyo kuendelea katika maeneo mengi zaidi na theluji itaendelea kuanguka kwa kiwango kikubwa zaidi mjini Kiev, hii leo.
Aidha, Utabiri wa hali ya hewa unaonesha mji wa Berlin hapa Ujerumani utapatwa na theluji kali na baridi itafikia nyuzi joto za selisiasi kumi chini ya sifuri.
Na hofu zaidi inapanda kwa watu wasiokuwa na makazi hasa wale wanaoishi mitaani na kulala barabarani. Shirikisho la Kimataifa la Msalaba Mwekundu na jumuiya zake ziko katika harakati za kuwatafutia ufumbuzi watu hao.
Mwakilishi wa shirikisho hilo Zlatko Kovac, ameliambia Shirika la Habari la Ufaransa kuwa watu hao wasio na makazi wamejikuta taabani na bila tahadhari yoyote na wako katika hali mbaya kwa sasa.
Nchi zilizoathirika na baridi hilo ni pamoja na Italia, Poland, Ukraine, Bulgaria, Romania, Ujerumani, Uingereza na Urusi.
Mwandishi: Pendo Paul\AFP
Mhariri: Yusuf Saumu