1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barcelona yateleza katika ligi ya Uhispania

19 Aprili 2016

Suala linalogonga vichwa vya habari ni mabingwa watetezi wa La Liga na mabingwa wa zamani wa Champions League Barcelona. Walipoteza mchuano wa tatu mfululizo

https://p.dw.com/p/1IYgs
Fußball FC Barcelona
Picha: picture-alliance/dpa/Q. Garcia

Kikosi hicho hatari cha kocha Luis Enrique kimekwama katika vungu la mchanga baharini na kukubali kipigo chake cha tatu mfulizo katika La Liga cha mabao 2-1 dhidi ya Valencia, wakati Atletico Madrid iliyoionyesha mlango Barca wa kutokea katika robo fainali ya Champions League wiki iliyopita imeendelea kupeta kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Granada na kukaa katika kiti kimoja cha usukani wa ligi hiyo pamoja na Barcelona.

Barca ina pointi 76 pamoja na Atletico, wakati Real Madrid inanyemelea nafasi ya ubingwa kwa kukaa pointi moja tu nyuma ya viongozi hao.

Leicester yaendelea kuongoza Premier Legaue

Leicester City ilitoka sare ya mabao 2-2 na West Ham United na kufungua mwanya wa pointi nane juu kileleni mwa Premier League ya Uingereza.

Wakati huo huo kocha wa Leicester City Claudio Ranieri amedai kitendo cha timu yake kuepuka kipigo dakika ya mwisho dhidi ya West Ham kinaweza kuimarisha imani ya wachezaji wake kwamba wanaweza kuwa mabingwa wa ligi ya Uingereza.

Großbritannien Fussball Robert Huth
Leicester City inanusia taji la Premier LeaguePicha: Getty Images/M. Regan

Mapambano ya katikati ya wiki katika Premier League yatatoa mwelekeo wa timu gani itaungana na Leicester City na Tottenham Hot Spurs katika timu nne zitakazoshiriki katika ligi ya mabingwa mwakani kutoka Uingereza. mapambano ya timu mbili nyingine zitakazojiunga na kuwa timu nne za Champions League yatakuwa kati ya Manchester City, Arsenal, Manchester United na West Ham United.

City na Arsenal zina pointi 60, nne zaidi ya Manchester United na West Ham, na zote zina michezo mitano kabla ya kufungwa janvi la ligi. City iko nyumbani kwa Newcastle kesho Jumanne wakati West Ham inaikaribisha Watford na United iko nyumbani ikiikaribisha Crystal Palace siku ya Jumatano. Na kisha Arsenal itakabiliana na West Bromwitch Albion siku ya Alhamis.

Juventus yatamba Italia

Juventus Turin imejiimarisha katika uongozi wa ligi ya Italia Serie A kwa ushindi wa mabao 4-0 nyumbani dhidi ya parlemo na kufungua mwanya wa pointi 9 kutoka kwa timu ya pili Napoli , ambapo timu hiyo ilipoteza mchezo wake kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Inter Milan.

Jana Jumapili Cristian Brocchi alianza vizuri muhula wa kuifunza AC Milan kwa kuiwezesha timu hiyo kupata ushindi wake wa kwanza katika michezo sita, na kisha kumshukuru Sinisa Mihajlovic baada ya kuchukua nafasi ya raia huyo wa Serbia kuifunza timu hiyo kigogo cha ligi ya Italia.

Milan ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Samdoria hali iliyoiweka matumaini ya timu hiyo hai ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao. Robert Lewandowski wa Bayern Munich anaelekeza nguvu zake katika kuongeza wingi wa mabao aliyoweka wavuni wakati Bayern Munich ikisaka nafasi katika fainali ya kombe la Ujerumani DFB Pokal katika mchezo wa nusu fainali utakaofanyika kesho Jumanne dhidi ya Werder Bremen.

Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / afpe / dpae / rtre
Mhariri: Josephat Charo