1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barcelona yashinda mchezo wa kwanza wa nusu fainali

Sekione Kitojo28 Aprili 2011

Barcelona ina nafasi kubwa ya kufikia fainali yao ya tatu ya Champions League katika muda wa miaka mitano baada ya kuwashinda mahasimu wao wakubwa Real Madrid

https://p.dw.com/p/1150k
Lassana Diarra wa Real katikati akipambana na Seydou Keita wa Barcelona na Pedro Rodriguez,kuliaPicha: dapd

Barcelona wananafasi nzuri ya kufikia fainali yao ya tatu ya Champions League katika muda wa miaka mitano baada ya kuwashinda mahasimu wao wakubwa Real Madrid kwa mabao 2-0 jana Jumatano katika mchezo ambao haukuwa wa kupendeza , uliojaa hasira, wa nusu fainali.

Mchezaji bora wa mwaka wa shirikisho la kandanda duniani FIFA, Lionel Messi aliweka wavuni mabao mawili kwa Barca baada ya mbinu ya Real Madrid ya kulinda lango na kushambulia kwa haraka kushindwa kufanyakazi safari hii, baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu mlinzi Pepe wa Real.

Kocha wa Real Jose Mourinho naye alipatiwa kadi nyekundu kwa kulalamika, na baadaye kumshutumu vikali mwamuzi kutoka Ujerumani Wolfgang Stark.

Jose Mourinho Fußballtrainer des Jahres 2010
Kocha wa Real Madrid Jose MourinhoPicha: dapd

Nawapongeza Barcelona, amesema kocha huyo Mreno, lakini sielewi ni kwa nini Barcelona kila mara hupata msaada wa refa. Maisha yangu yote nitajiuliza swali hili, na siku moja natumai kupata jibu.

Mourinho alishangaza kusema kuwa ,tulikuwa tunatarajia sare ya bila kwa bila, lakini kutolewa Pepe , kuliwapa nafasi ya wazi Barcelona kutushinda. Sasa ni kazi pevu kwetu kuweza kushinda.

Kocha huyo raia wa Ureno amemaliza kwa kusema, Sisikitiki sana, nina familia nzuri. Lakini sielewi kwa nini Barcelona wana nguvu hizi. Imetokea miaka miwili iliyopita kwa Chelsea, katika nusu fainali mwaka 2009, na kisha karibu itokee kwa Inter yangu mwaka jana, na pia kwa Arsenal mwaka huu.

Kwa nini wapinzani wa Barcelona kila mara hutolewa mtu kwa kadi nyekundu ameuliza Mourinho. Nguvu hizi wanazipata wapi? Huenda ni kutoa matangazo zaidi kwa UNICEF, huenda ni kwasababu ya nguvu za rais wa shirikisho la kandanda la Hispania, Jose Angel Villar katika shirikisho la kandanda la Ulaya , UEFA.

Mkurugenzi mkuu wa Real ,Jorge Valdano kwa upande wake amesema, uamuzi wa kumtoa Pepe ulikuwa ni sababu kubwa, ni kitu pekee katika mchezo huo kilichokuwa muhimu kuliko Messi. Valdano ameongeza kuwa hakuna uwezekano wa kubadilisha matokeo haya huko mjini Barcelona, kwa sababu uwezo na historia ya club hii.

Mchezaji wa kiungo wa Real Xabi Alonso pia amesema , uamuzi wa kumtoa Pepe ulikuwa ndio kitu kilichoamua matokeo, ulibadilisha kila kitu.Najua siwezi kusema sipendelei upande wowote, lakini haikuwa kadi nyekundu ya moja kwa moja, hii inasikitisha.

Kocha wa Barca Pep Guardiola hakupenda kujibu shutuma za Mourinho. Amesema tu kwamba , tulicheza vizuri, kwa udhibiti wa hali ya juu wa mchezo. Na pia kwa nguvu kidogo. Nimefurahi sana na jinsi wachezaji wangu walivyocheza.

Der Trainer von Barcelona Pep Guardiola
Kocha wa Barcelona Pep GuardiolaPicha: AP

Wakati wa mapumziko mlinda mlango wa akiba wa Barcelona Jose Mauel Pinto alipewa kadi nyekundu kwa kupigana na wachezaji wa Real katika njia kuelekea katika vyumba vya kuvalia. Kwa jumla mwamuzi Wolfgang Stark alitoa kadi tano za njano na tatu nyekundu. Barca ilimiliki mpira kwa asilimia 71, wakati Real ikiridhika tu na kulinda lango lao na kujaribu kushambulia kwa kushtukiza. Mkakati huu uliwasaidia sana hapo Aprili 20 katika fainali ya kombe la Hispania na kushinda kwa bao 1-0, lakini ilishindwa kabisa mara hii.

Mwandishi : Sekione Kitojo / dpae