1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barcelona na Real watoana kijasho

7 Mei 2018

Watani wakubwa wa kandanda la Uhispania Barcelona na Real Madrid walionyesha kwamba hawahitaji kuwa katika kinyang'anyiro cha kuwania mataji  ndipo waweze kuonyesha burudani safi la kandanda.

https://p.dw.com/p/2xK2L
Spanien La Liga FC Barcelona v Real Madrid
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Fernandez

Watani wakubwa wa kandanda la Uhispania Barcelona na Real Madrid walionyesha jana kuwa hawahitaji kuwa katika kinyang'anyiro cha kuwania mataji  ndipo waweze kuonyesha burudani safi la kandanda. Huku Barca wakiwa tayari wameshinda ubingwa wa La Liga, nao Madrid wakiangaza macho yao kwa fainali ya Champions League baadaye mwezi huu, ilitarajiwa kuwa mechi ya el Classico isiyo na mvuto wowote katika miaka mingi.

Badala yake, uwanja wa Camp Nou ulishuhudia mpambano wenye hisia kali na mabao manne, ukiwemo mkwaju wa Lionel Messi uliohakikisha kuwa Barca wanapata sare ya 2-2 na kuwa timu pekee ambayo haijapoteza mechi yoyote kwenye ligi msimu huu. Ronaldo pia alifunga licha ya kuwa alionekana kuumia.

Kulikuwa na kadi nane za njano na moja ya nyekundu wakati mchezaji wa Barca Sergi Roberto alipotimuliwa uwanjani kwa kadi ya pili ya njano. Timu zote hazikufurahia kazi ya refarii. Zinedine Zidane ni kocha wa Real "kama kawaida, sitozungumzia waamuzi. nadhani tulicheza vizuri hasa katika kipindi cha kwanza wakati tulikuwa wachezaji 11 kila upande. tulicheza vyema na kutengeneza nafasi. hatukuweza kufunga bao na katika kipindi cha pili ikawa wachezaji 10 dhidi ya 11 na hali ikawa mbaya sana kwetu. Sijui, labda hatukuwa wabunifu sana katika hatua za mwisho, lakini hakuna kinachobadilika. hatukupoteza mechi. Naipongeza Barcelona"

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman