1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la usalama lazungumzia hali ya hewa

Maja Dreyer17 Aprili 2007

Kwa mara ya kwanza katika historia yake, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linazungumzia suala la mabadiliko ya hali ya hewa. Uingereza hasa imejitahidi suala hilo liwekwe kwenye ratiba ya baraza ambalo jukumu lake ni kushughulikia masuala yanayohusiana na usalama wa dunia. Mabadiliko ya hali ya hewa lakini ndiyo hatari kubwa kwa usalama, anasema waziri wa nchi za nje wa Uingereza, Bi Magret Beckett, ambaye ataongoza mjadala huo.

https://p.dw.com/p/CHG4
Ukame kama nchini Kenya unaweza kutokea mara nyingi zaidi
Ukame kama nchini Kenya unaweza kutokea mara nyingi zaidiPicha: DW /Maya Dreyer

Mada ya mjadala wa leo kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ni “Nishati, usalama na hali ya hewa” - kama ilivyopendekezwa na Uingereza ambayo kwa mwezi huu inachukua zama ya mwenyekiti wa baraza hilo. Mwanadiplomasia mmoja wa Kiingereza ambaye hakutaja jina lake litajwe alisema lengo la mjadala huo ni kuzidi kutambua tatizo hilo ambalo linazidi kupata umuhimu kwenye uwanja wa kimataifa. Alisema pia kwa mtazamo wa Uingereza, gharama za kuchukua hatua sasa ni ndogo kuliko gharama za athari kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.


Athari za mabadiliko ya hali ya hewa ziliwekwa wazi hivi karibuni tu katika ripoti kubwa ya Umoja wa Mataifa iliyoandikwa na zaidi ya wanasayansi 450 na ambayo inaonya kuwa hadi asilimia 30 ya viumbe wanyama na mimea wanaweza kuangamizwa kutokana na ongezeko la joto duniani. Matokeo mengine yataweza kuwa vipindi virefu vya joto, mafuriko, dhoruba kali na ukame, ripoti hii inasema.

Ndiyo maana pia ni suala la usalama ulimwenguni na changamoto kubwa zaidi ya karne hii. Wanasayansi wengine wameonya kutokea mizozo ya mipaka, juu ya maji au ardhi, majanga ya njaa au uhamiaji wa watu wengi kutokana na athari za ongezeko la joto. Au, kama alivyoeleza balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa Emyr Jones-Parry, usalama wa nchi kadhaa uko hatarini ikwa watu wanaokaa katika maeneo ya pwani watalazimika kuhama kwenye maeneo ya nyanda za juu kutokana na kupanda wa kima cha maji.

Uchina na Urusi, nchi mbili kati ya nchi tano zenye kura ya turufu zilikuwa na wasiwasi juu na suala hilo kuzungumziwa katika baraza la usalama, kama ilivyosikika katika duru za kidiplomasia. Marekani pia ilisema hivyo, lakini Jumatatu kulitolewa ripoti iliyoandaliwa na wakuu na majenerali wa jeshi la Marekani waliostaafu ambayo inasema mabadiliko ya hali ya hewa duniani ni hatari kubwa nchini Marekani, kwenye operesheni za kijeshi na pia kuongezeka mizozo ya kimataifa.

Mjadala katika baraza la usalama unatarajiwa kuhusu zaidi athari za hali ya hewa kwa amani na usalama duniani pamoja na kutafuta njia vipi baraza hili linavyoweza kuzuia mizozo inayotokana na mabadiliko ya hali ya hewa na jinsi jumuiya ya kimataifa inavyoweza kuzisaidia nchi husika. Baraza la usalama lakini halitarajiwi kupitisha azimio.

Balozi wa Uingereza Jones-Parry anatumai Umoja wa Mataifa utaandaa mkutano wa kilele kuhusiana na hali ya hewa mwakani. Katibu mkuu wa Umoja huu, Ban Ki Moon, katika mahojiano na gazeti la “Financial Times” ameshataja kufanya mkutano wa vyeo vya juu kutafuta muelekeo wa kisiasa kwa mkutano wa aina hiyo. Kwanza lakini anataka kuzungumzia suala hilo kwenye mkutano wa nchi nane zilizostawi kiviwanda duniani, G8, utakaofanyika mwezi wa June nchini Ujerumani.