Baraza la Usalama latakiwa kuchukua hatua DRCongo
4 Oktoba 2013Vitendo hivyo vinavyotokea hivyo vya kihalifu na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu vinatokea bila ya watendaji kujali kuwa watashitakiwa katika eneo hilo la mashariki ya jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo.
Wajumbe wa baraza la Usalama walitarajiwa kusafiri kwenda katika maeneo hayo kuanzia jana Oktoba 3 kwa ziara ya siku 6 nchini Congo, Rwanda, Uganda, na Ethiopia. Sekione Kitojo na taarifa zaidi.
Barua hiyo iliyotumwa Oktoba 2, 2013 katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa , imeeleza kuwa raia katika eneo la mashariki mwa jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo wanaathirika na vitendo vya kikatili visivyokwisha , lakini ni wachache kali ya wale wanaohusika na vitendo hivyo ambao wanafikishwa mbele ya haki, amesema Daniel Bekele , mkurugenzi wa shirika la Human Rights Watch katika Afrika.
Mbinyo zaidi
Wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wanapaswa kutumia ziara yao hii kuziwekea mbinyo serikali katika eneo hilo kufikisha mwisho uungaji mkono wa aina yoyote kwa makundi yenye silaha ambayo yanaendesha vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu na kuwakamata watuhumiwa wa uhalifu wa kivita.
Shirika la Human Rights Watch limesema katika barua hiyo pia kuwa baraza la usalama linapaswa kuidhinisha azimio litakaloitaka Rwanda kusitisha misaada yake kwa kundi la waasi la M23, kundi ambalo linafanya vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu na ambalo linahusika na vitendo kadha vya kikatili katika eneo la mashariki mwa jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, na kuweka vikwazo dhidi ya maafisa wa ngazi ya juu wa serikali ya Rwanda ambao wanahusika katika kuwasaidia waasi hao.
Mwanamke mmoja kutoka mji wa Rutshuru amewaambia watafiti wa shirika hilo la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch wiki hii kuwa amebakwa na mpiganaji wa kundi la waasi la M23, ambae alimwambia , "Sisi pia tuna wake zetu, lakini wamebaki Rwanda. Kwa hiyo ndio sababu nimekubaka..." Baada ya kumbaka mwanamke huyo , mpiganaji huyo alimpiga risasi katika mapaja yake.
Mazungumzo yamekwama
Serikali ya Kongo na kundi la M23 wamekuwa na mazungumzo ambayo yamekwama mjini Kampala, Uganda , tangu mwezi Desemba 2012.
Makubaliano yaliyopita kati ya serikali ya Kongo na makundi mengine ya watu wenye silaha yameruhusu makamanda wa waasi ambao wanahusika na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na vitendo vya kikatili kuzawadiwa kwa vitendo vyao hivyo kwa kuingizwa katika jeshi la Kongo.
Wengi wa makamanda hawa wamekuwa wakiendelea na vitendo vyao vya kikatili dhidi ya raia wakati wakiwa maafisa katika jeshi la Kongo na baadaye wakaazisha uasi mpya, limesema shirika hilo la Human Rights Watch.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo , MONUSCO, unapaswa kufanya kila juhudi kuwalinda raia dhidi ya kitisho kinachowakabili cha kundi la M23 na makundi mengine yenye silaha. Human Rights Watch imesema kuwa ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani unapaswa kuchukua tahadhari kwa kundi la wapiganaji wa Ntabo Ntaberi Sheka, ambalo wapiganaji wake wameua, wamebaka , na kuwakata viungo raia kadha tangu Mei 2013. Septemba 27, walishambulia vijiji kadha katika eneo la Masisi, na kuua watoto, kuwabaka wanawake na kuchoma nyumba.
Wanajeshi wa jeshi la Kongo pia wanahusika na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na ubakaji wa wanawake wapatao 76 na wasichana nje na ndani ya mji wa Minova, katika jimbo la Kivu ya kusini Novemba mwaka 2012.
Mwandishi : Sekione Kitojo / Human Rights Watch
Mhariri: Josephat Charo