1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la usalama lashindwa kuamua juu ya kutotambua matokeo ya uchaguzi Zimbabwe

28 Juni 2008

-

https://p.dw.com/p/ESIf

Harare

Shughuli ya kuhesabu kura inaendelea nchini Zimbabwe pamoja na kwamba mshindi anajulikana wazi ni rais Mugabe baada ya mgombea wa chama cha upinzani cha MDC Morgan Tsvangirai kujitoa kwenye kinyang'anyiro hicho cha duru ya pili kupinga kile alichosema ni kitisho na ghasia dhidi ya wafuasi wake.Uchaguzi wa duru ya pili umefanyika licha ya kutolewa miito na jumuiya ya kimataifa ya kutaka uhairishwe. Wasimamizi wa uchaguzi wamefahamisha kwamba idadi ya waliojitokeza kupiga kura hapo jana ilikuwa ndogo mno ingawa gazeti rasmi la serikali limesema kwamba idadi hiyo ilikuwa ya kuridhisha.Baraza la usalama la Umoja wa mataifa limetangaza masikitiko yake juu ya kufanyika uchaguzi huo likisema uchaguzi huo umefanyika chini ya mazingira ambayo hayana usawa.Hata hivyo baadhi ya wajumbe wa nchi za magharibi wamevunjwa moyo na baraza la usalama kutokana na kushindwa kufikia uamuzi wa pamoja wa kuharamisha matokeo ya uchaguzi wa Zimbabwe baada ya Afrika Kusini kupinga hatua hiyo.Balozi wake katika Umoja wa mataifa Dumisani Kumalo amesema isubiriwe hadi baada ya mkutano wa kilele wa wakuu wa Umoja wa Afrika. Aidha Kumalo amesema baraza la usalama halina haki ya kuingilia masuala ya ndani ya Zimbabwe. Uingereza pamoja na Marekani zimeshasema hazitayatambua matokeo ya uchaguzi wa Zimbabwe. Kwa upande mwingine balozi wa Marekani katika Umoja wa mataifa Zalmy Khalilzad amesema nchi yake imeanzisha mazungumzo na baadhi ya wanachama wengine wa baraza hilo la usalama juu ya uwezekano wa kuiwekea vikwazo Zimbabwe ingawa huenda baraza hilo likashindwa kupitisha vikwazo vyoyvote kutokana na upinzani wa Afrika Kusini,China na Urussi. Wakati huohuo mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika Jean Ping amewaambia mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja huo kuwaachia marais wa nchi za Umoja wa Afrika watoe uamuzi wao juu ya mzozo huo wa Zimbabwe watakapokutana kwenye mkutano wao wa kilele wiki ijayo. Aidha duru za tume ya Umoja wa Afrika zimedokeza kuwa baraza la amani na usalama la Umoja huo litafanya kikao maalum kuijadili Zimbabwe kesho jumapili huko Sharm El Sheikh Misri.