UN yakataa ombi la Marekani kuirejeshea vikwazo Iran
26 Agosti 2020Balozi wa Indonesia katika Umoja wa Mataifa ambaye kwa sasa ndiye rais wa kupokezana wa Baraza la Usalama, Dian Triansyah Djani, alitoa tangazo hilo kufuatia maombi ya Urusi na China kutaka matokeo ya kura ya maoni ya wanachama wote 15 wa baraza hilo kuhusu ombi la Marekani yatangazwe.
Alhamis iliyopita (Agosti 20), Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo alisisitiza kuwa Marekani ina haki kisheria kuvirudisha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran, licha kuwa Rais Donald Trump alishaiondoa nchi yake kwenye mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 kati ya Iran na nchi nyingine sita zenye nguvu kubwa ulimwenguni, ambao uliidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Wanachama wote isipokuwa Jamhuri ya Dominika, walimwambia rais wa baraza hilo kwamba hatua za utawala wa Marekani ni kinyume cha sheria kwa sababu mnamo mwaka 2018 Trump alijiondoa kwenye mkataba huo uitwao kwa kifupi JCPOA.
Djani aliwaambia wanachama wa Baraza lake wakati wa mkutano kwa njia ya video siku ya Jumanne (Agosti 25) kwamba hakuna makubaliano ya pamoja kuhusu suala hilo, kwani wanachama wengi wamepinga isipokuwa mmoja na kwa hivyo hawezi "kuchukua hatua zaidi."
Hiyo ilimaanisha kwamba Baraza hilo lenye nguvu zaidi katika Umoja wa Mataifa lisingeliridhia matakwa ya Marekani, angalau katika kipindi ambacho baraza hilo linaongozwa na Indonesia.
Mataifa ya Afrika yaipinga Marekani
Niger inatarajiwa kuchukua urais wa kupokezana wa baraza hilo mwezi Septemba, na tayari balozi wake aliandika barua ya pamoja na Afrika Kusini na Tunisia, ambapo walisema Marekani haina uwezo wa kurudisha vikwazo dhidi ya Iran kwa kuwa si mwanachama tena wa JCPOA.
Baadaye, ujumbe wa Marekani katika Umoja wa Mataifa ulituma taarifa ukisema Marekani imejikita katika msingi imara wa kisheria kuanzisha hatua za kurudisha vikwazo hivyo dhidi ya Iran chini ya makubaliano ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaliyoidhinisha mkataba wa 2015 kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
Siku ya Jumanne (Agosti 25), Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Kelly Craft alirejelea ujumbe wa Pompeo uliosema kuwa Marekani isingeliruhusu "nchi ambayo ni mfadhili mkubwa wa ugaidi ulimwenguni kuwa na uhuru wa kununua na kuuza ndege, vifaru, makombora na zana nyingine za kivita kumiliki silaha za nyuklia".
Urusi, China zasifia uamuzi wa Baraza la Usalama
Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia aliusifia uamuzi wa rais wa baraza la usalama akisema ni hatua nzuri.
Balozi wa China katika umoja huo, Zhang Jun, pia aliutaja uamuzi wa Djani kuwa hatua muafaka yenye mwelekeo sawa.
Naibu balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, Anne Gueguen, alisema nchi wanachama 13 kati ya 15 wa baraza hilo, zikiwemo nchi tatu za Ulaya, ambao bado ni wanachama wa JCPOA, zinakubaliana kwamba Marekani si mshirika tena katika mkataba wa Iran na "kwa hivyo matakwa yake ya kurudisha vikwazo hayana maana."
Ujumbe wa Iran ulisema majadiliano ya baraza hilo yalionesha kwa mara nyingine hali ya Marekani kujitenga katika JCPOA.
Taarifa ya ujumbe huo iliongeza kwamba Iran ilikuwa inaamini wanachama wa baraza hilo wangeliendelea kuizuia nchi hiyo dhidi ya kuuhujumu Umoja wa Mataifa ikiwemo Baraza lake la Usalama.
Vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran vilipaswa kumalizika Oktoba 18.