Baraza la Usalama lajadili haki za binadamu Korea Kaskazini
23 Desemba 2014Msaidizi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa masuala ya Haki za Binaadamu Ivan Simonovic ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York hapo Jumatatu kwamba ni nadra sana kwa orodha kubwa ya madai mazito ya uhalifu wa kimataifa kuwasilishwa kwenye baraza hilo.
Mkutano wa baraza hilo kuhusu Korea Kaskazini umefanyika baada ya kutumika kwa utaratibu wa kupiga kura wa aina yake kutokana na China kupinga kuingizwa kwa suala hilo la Korea Kaskazini katika agenda ya baraza hilo.
Kura 11 ziliunga mkono,mbili zilipinga na wajumbe wawili hawakushiriki kupiga kura.Urusi na China zilipiga kura dhidi ya kuingizwa kwa suala hilo katika agenda ya baraza lakini kutokana na kwamba hakuna utaratibu wa kura za turufu kwenye utaratibu uliotumika kupiga kura jaribio la China kutaka kulizima suala hilo limeshindwa.
Pingamizi ya China
Kabla ya kupigwa kwa kura hiyo balozi wa China kwenye Umoja wa Mataifa Liu Jieyi amesema Baraza la Usalama sio kikao cha kujihusisha na masuala ya haki za binaadamu na linapaswa kujiepeusha na hatua yoyote ile ambayo yumkini ikazidi kulichochochea suala hilo.
Korea Kaskazini yenyewe imeususia mkutano huo na kuonya kwamba maamuzi juu ya namna ya kukabiliana na jambo hilo yatatolewa mjini Pyongyang.
Baada ya kupigwa kwa kura hiyo mkutano rasmi juu ya Korea Kaskazini ulianza kama ilivyoombwa na balozi wa Australia Gary Quinian na mabalozi wengine tisa wengi wao wakiwa wa mataifa ya magharibi.Quinian alielezea hatua ya baraza hilo kuwa ya kihistoria.
Taifa la kidikteta
Amesema Jamhuri ya Kidemokrasia ya Wananchi wa Korea DPRK yaani Korea Kaskazini kwa kweli ni taifa la kidikteta ambalo hutumia matumizi ya nguvu, ukandamizaji na asasi za kijeshi dhidi ya raia wake yenyewe ili kuweza kuendelea kubakia madarakani.
Ameongeza kusema ukatili wa utawala huo dhidi ya wananchi wake umelifanya taifa hilo kukosa utengamano.
Balozi wa Marekani kwa Umoja wa Mataifa Samantha Power ameelezea maisha ya Korea Kaskazini kuwa jinamizi na kupuuzilia mbali kama ni upumbavu madai ya Korea Kaskazini kutaka ufanyike uchunguzi wa pamoja wa udukuzi wa kampuni ya Marekani ya Sony Pictures na vitisho vya kulipiza kisasi iwapo Marekani itagoma kufanya hivyo kufuatia kisa cha udukuzi kutokana na filamu iliogiza jaribio la kuuwawa kwa kiongozi wa Korea Kaskazini.
Mkutana huo umekuja baada Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hapo Ijumaa kulitaka Baraza la Usalama la Umoja wa huo kufikiria kuifikisha Korea Kaskazini katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa uhalifu dhidi ya ubinaadmu kama ilivyodaiwa katika repoti ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa mwezi wa Februari.
Mara ya mwisho Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupiga kura ya utaratibu kama hiyo ilikuwa mwaka 2006 wakati ilipoiongeza Myanmar kwenye agenda yake.Hadi sasa mazungumzo ya baraza hilo kuhusu Korea Kaskazini yamekuwa tu kwenye suala la mpango wake wa nyuklia tu.Lakini kutokana na kura hiyo fani zote za nchi hiyo zinaweza kufanyiwa uchunguzi.
Mwandishi. Mohamed Dahman/Reuters /dpa
Mhariri: Gakuba Daniel