1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili - Madaya

15 Januari 2016

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajia kuwa na kikao cha dharura katika kujaribu kuzishawishi pande zinazohusika na mgogoro wa kisiasa nchini Syria kuacha kuyazingira baadhi ya maneo nchini humo.

https://p.dw.com/p/1He5V
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: picture-alliance/Geisler-Fotopress/D. van Tine

Hatua hiyo inakuja wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akitoa mwito wa kuzitaka pande zote zinazohusika na mgogoro nchini humo ikiwa ni pamoja na upande wa serikali ya Syria na ule wa waasi kuacha mara moja kuyazingira maeneo hayo zikiwa zimesalia siku kadhaa kuelekea mazungumzo ya amani kujadili mgogoro huo wa Syria hapo Jan. 25 , mwaka huu mjini Geneva Uswisi.

Mji wa Madaya umekuwa ukizingirwa kwa miezi kadhaa sasa na majeshi ya serikali ya Rais Bashar al-Assad wakati miji mingine miwili ya Foua na Kifarya imezingirwa na waasi. Akizungumza mara baada ya kuhutubia mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa ambako alielezea vipaumbele vyake kwa mwaka 2016, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alionesha kusikitishwa kwake na hali ya maisha ya watu katika maeneo yaliyozingirwa ambao wanaonekana kudhoofika kutokana na kukosa chakula pamoja na mahitaji mengine muhimu ya kibinadamu.

Katibu Mkuu Ban Ki-moon alisema Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kibinaadamu yana uwezo wa kugawa vyakula kwa asilimia moja tu ya watu waliozingirwa nchini Syria na kuongeza kuwa pande zote nchini humo ambazo ni serikali na upande wa waasi zinafanya uhalifu wa kivita kwa kusababisha njaa kwa makusidi kwa raia wa nchi hiyo wasiyo na hatia na kuwa wote wanaohusika na tatizo hilo watakabiliwa na mkono wa sheria.

Hali ya maisha ya watu katika eneo la Madaya ni mbaya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliongeza kuwa kiasi ya watu 400 wanaume , wanawake na watoto katika mji wa Madaya wako katika hali mbaya wakikabiliwa na utapia mlo na matatizo mengine ya hali ya kibinadamu na kuwa katika hatari ya kupoteza maisha na hivyo kuhitaji huduma za kiafya mapema iwezekanavyo ikiwa ni pamoja na kuhamishwa kutoka katika maeneo hayo kwa sasa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.Picha: picture-alliance/Photoshot/Xinhua/L. Muzi

Aidha, shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya watoto UNICEF katika taarifa yake hii leo limethibitisha juu ya hali mbaya ya utapiamlo inayowakabili baadhi ya watoto katika mji wa Madaya ambako misaada ya mahitaji muhimu ya kibinadamu iligawiwa juma hili kwa maelfu ya watu ambao wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu kwa mwezi mmoja sasa. UNICEF katika taarifa yake hiyo imedai kushuhudia kifo cha mtoto mwenye umri wa miaka 16 katika eneo hilo ambaye alikuwa akikabiliwa na tatizo la utapia mlo.

Mapema juma hili mjumbe wa Syria katika Umoja wa Mataifa Bashar Ja afari alizipuuza taarifa hizo za watu kukabiliwa na njaa katika mji wa Madaya akisema ni uongo mtupu.

Mwandishi: Isaac Gamba/APE/ RTRE

Mhariri: Iddi Ssessanga