Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuijadili Mali
14 Januari 2013Nchi kadhaa za Umoja wa Ulaya na Marekani zinaiunga mkono Ufaransa. Lakini Ujerumani imesema haitashiriki katika harakati za kijeshi nchini Mali. Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle amesema suala hilo halipo. Msemaji wa ubalozi wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa Ufaransa imeitisha kikao hicho ili kupeana taarifa na mawazo.
Lakini Radio ya Ufaransa-RFI imearifu kwamba harakati za kijeshi za Ufaransa, nchini Mali pamoja na hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kuleta utulivu nchini Mali ni miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa kwenye kikao hicho cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kikao cha Baraza la Usalama kinafanyika wakati ndege za Ufaransa zimefanya mashambulio kwenye ngome za waasi wenye itikadi kali ya Kiislamu kwa siku ya tatu mfululizo nchini Mali.
Ufaransa yadhamiria kuharakisha kupelekwa wanajeshi 3,300
Ufaransa inadhamiria kuliharakisha zoezi la kuwapeleka nchini Mali wanajeshi elfu tatu na mia tatu kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi-Ecowas. Kimsingi Barala la Usalama la Umoja wa Mataifa liliridhia kupelekwa kwa wanajeshi hao nchini Mali mwezi Desemba mwaka jana. Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia eneo la Sahel, Romano Prodi ametetea hatua za kijeshi zinazochukuliwa na Ufaransa nchini Mali.
Mjumbe huyo ameliambia gazeti la "Die Welt" kwamba hatua ya Ufaransa inaungwa mkono kwa kiwango kikubwa. Mjumbe huyo ameeleza kuwa wote wana hofu juu ya magaidi wenye itikadi kali ya Kiislamu. Naye Waziri wa Mambo ya nje wa Ufaransa L. Fabius ametilia maanani uungaji mkono wa Uingereza na Denmark. Nchi hizo zinaiunga mkono Ufaransa katika mambo ya usafirishaji.
Ujerumani bado yajitafakari
Ama kwa upande mwingine Ujerumani imesema haitashiriki katika harakati za kijeshi nchini Mali. Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Guido Westrewelle ameeleza kuwa suala la nchi yake kushiriki katika mapambano nchini Mali halimo kabisa katika ajenda. Amesema kushiriki kwa wanajeshi wa Ujerumani nchini Mali siyo suala kuzungumziwa asilani, lakini bado wanatafakari namna ya kuunga mkono mchakato wa kisiasa.
Hata hivyo, msemaji wa masuala ya nje wa chama cha CDU kinachoongoza serikali ya mseto ya Ujerumani, Ruprecht Polenz ameeleza kuwa jeshi la Ujerumani linaweza kushiriki katika mgogoro wa Mali kama sehemu ya Umoja wa Ulaya. Bwana Polenz amesema ikiwa Mkuu wa sera za nje wa Umoja huo Catherine Ashton atawasilisha mipango ya busara, Ujerumani haitaweza kujiweka kando. Umoja wa Ulaya unafikiria kupelaka wanajeshi 200 nchini Mali.
Naye msemaji wa masuala ya ulinzi wa chama kikuu cha upinzani nchini Ujerumani Rainer Arnold amesema Ujerumani inapaswa kuiunga mkono Ufaransa kijeshi nchini Mali. Bwana Rainer amesema endapo maombi yatatolewa, Ujerumani itapaswa kutafakari kwa makini sana juu ya kuiunga mkono Ufaransa katika masuala ya ugavi na usfirishaji. Lakini Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Thomas de Maizere ametamka wazi kuwa Ujerumani inaweza kushiriki katika mgogoro wa Mali kwa sharti la kutoingia katika mapambano.
Mwandishi:Mtullya Abdu/AFPD
Mhariri:Hamidou Oummilkheir