1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuidhinisha taarifa ya pamoja dhidi ya Korea Kaskazini.

Nina Markgraf13 Aprili 2009

Baraza la usalama la umoja wa mataifa linatarajiwa kuidhinisha taarifa ya pamoja , inayoishtumu, Korea Kaskazini kwa kufyatua roketi yake ya masafa marefu.

https://p.dw.com/p/HVr7
Balozi wa Marekani, katika Umoja wa Mataifa.Picha: AP


Taarifa hiyo pia inataka kuendelezwa kwa vikwazo dhidi ya Pyong Yang.

Kim Jong Il Machthaber Nord Korea
Rais wa Korea Kaskazini, Kim Jong IlPicha: AP

Ingawa si azimio ambalo lingekuwa na uzito mkubwa, taarifa hii ya pamoja ya kulaani hatua ya Korea Kaskazini kufyatua kombora la masafa marefu, ilikubaliwa Jumamosi, katika mkutano wa faragha baina ya wanachama watano wa kudumu wa baraza la usalama la umoja wa Mataifa, Uingereza, China, Ufaransa, Urusi na Marekani. Japan pia ilishirikishwa.


Baadaye taarifa hii iliwasilishwa kwa nchi wanachama wengine kumi ambao sio wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.


Kulingana na Mwenyekiti wa mwezi huu, wa baraza hilo la usalama, Claude Heller, ambaye pia ni balozi wa Mexico, katika Umoja wa Mataifa- taarifa hii iliowasilishwa na balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Susan Rice- ni ishara tosha kuwa Baraza la Usalama halikuridhishwa na kitendo cha Korea Kaskazini.


Japan imekuwa mstari wa mbele kuwasilisha malalamishi yake na kutaka Pyong Yang ichukuliwe hatua.


Rice aliwaambia waandishi wa habari kwamba ana imani baraza la usalama litaidhinisha taarifa hii, ili iwe funzo kwa Korea Kaskazini kwamba kitendo chao cha kufyatua kombora la masafa marefu kwa kisingizio kuwa walikuwa wanapeleka satelite angani, hakitokubalika. Na kwamba unapovunja sheria, inabidi ubebe dhamana.


Na haitokuwa tu kulaani hatua ya Pyonga Yang, hatua ya baraza la uslama pia inalenga kuendelezwa kwa vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini kutokana na kukiuka azimio la Umoja huo la 1718.Vikwazo hivi ni pamoja na marufuku ya kuingizwa bidhaa au kusafirishwa nje kwa bidhaa kutoka Korea Kaskazini.


Taarifa hiyo ya pamoja iliyoletwa mbele ya baraza hilo na Marekani pia inatoa mwito wa njia zote za kidiplomasia kuchukuliwa ili kutatua swala hili kupitia mazungumzo ya mataifa sita. Mazungumzo hayo yanazijumuisha nchi za China, Marekani, Korea Kusini, Japan na Urusi.


Lakini tangu desemba mwaka jana mazungumzo yalikwama baada ya utawala wa Kim Jong Ill kukataa kutoa wazi taarifa zozote kuhusiana na mpango wake wa kutengeneza silaha za kinuklia.


Pale Pyong Yang ilipokaidi jumiya ya kimataifa, na kufyatua kombora lake, Marekani, Japan, Ufaransa na Uingereza zilitaka hatua kali ichukuliwe dhidi ya utawala huu wa kikoministi. China na Urusi hata hivyo ziliitoa mwito wa subira, ili hatua zitakazochukuliwa zisidhuru harakati za kuanzisha upya mazungumzo ya nchi sita.


Kwa taarifa yeyote ya pamoja kupitishwa katika baraza la usalama la umoja wa mataifa, ni lazima iungwe mkono na wanachama wote 15 wa baraza hilo. Inatabiriwa taarifa hii ya pamoja ya kuishtumu Korea Kaskazini haitakuwa na pingamizi kutokana na kuungwa mkono na mataifa yote matano yenye ushawishi mkuu. Gazeti la New York Times liliripoti kwamba Libya, ambayo si mwanchama wa kudumu wa baraza la usalama imeonekana haikuridhishwa na taarifa hii ikisema, kupeleka satelite ya mawasiliano katika anga za juu ni haki ya kila nchi.


Mwandishi Munira Mohammed/AFPE

Mhariri Saumu Mwasimba