Baraza la Usalama kupigia kura azimio kuhusu Syria
23 Februari 2018Haijabainika wazi iwapo kura hiyo itakayopigwa leo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa inaungwa mkono na Urusi ambayo ni mshirika wa karibu wa Syria.
Urusi hapo jana, ililiambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa bado hakuna makubaliano yaliyofikiwa ya kusitishwa mapigano kwa siku 30 nchini Syria, tamko ambalo limedidimiza matumaini ya kusitisha mashambulizi makali yanayoendelea katika eneo linalodhibitiwa na waasi la Mashariki mwa Ghouta.
Urusi yashutumiwa kwa kuikingia kifua Syria
Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia aliwasilisha vipengee vipya kujumuishwa katika rasimu ya azimio kuhusu Syria. Ili azimio lipitishwe, linapaswa kuungwa mkono kwa kura tisa bila ya kupingwa kwa kura ya turufu kutoka nchi wanachama wa kudumu Urusi, China, Marekani, Uingereza na Ufaransa.
Urusi imetumia mara 11 kura yake ya turufu kuzuia Baraza hilo la Usalama kuuchukulia hatua Syria tangu vita kuzuka nchini humo mwaka 2011.
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Marekani Heather Nauert ameishutumu Urusi kwa kushindwa kuepusha janga la kibinadamu Syria akisema Urusi inatwishwa jukumu la kipekee kutokana na hali inayojiri kwani bila ya usaidizi wao kwa utawala wa Rais Bashar al Assad, mauaji na dhiki havingetokea katika eneo hilo.
Mashambulizi makali yameshuhudiwa Mashariki mwa Ghouta, ngome pekee iliyosalia ya waasi tangu Jumapili. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterress ametoa wito kwa mapigano kusitishwa mara moja katika eneo hilo.
Idadi ya raia walioathirika ni kubwa
Mashambulizi mapya ya mabomu Mashariki mwa Ghouta jana yaliongeza idadi ya raia waliouawa na majeshi ya serikali hadi zaidi ya 400. Huku wanadiplomasia wakivutana kuhusu kura hiyo katika Umoja wa Mataifa, wakaazi wa eneo hilo wanatafuta kila mbinu ya kunusurika na kifo na majeraha kwa kujificha katika mahandaki kuepuka mashambulizi makali ya mabomu na maroketi kutoka kwa wanajeshi ambao pia wanashambulia mahospitali.
Shirika la madaktari wasio na mipaka MSF limesema vituo 13 inavyosimamia Mashariki mwa Ghouta vimeharibiwa katika kipindi cha siku tatu zilizopita na hivyo kufanya kazi ya kuwaokoa mamia ya watu waliojeruhiwa kuwa ngumu mno.
Shirika la kutetea haki za binadamu Syria limesema siku tano za mashambulizi zimesababisha vifo vya raia 403 wakiwemo watoto 95.
Mwandishi: Caro Robi/Reuters/afp
Mhariri: Yusra Buwayhid