Baraza la usalama kujadili mapinduzi ya Myanmar
2 Februari 2021Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litafanya mkutano wa dharura kujadili mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini Myanamar.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameyaeleza mapinduzi hayo kuwa ni pigo kubwa kwa demokrasia ya Myanmar.
Soma zaidi:Myanamar: Jeshi limetangaza hali ya dharura na kuchukua madaraka
Mkutano huo utakaofanyika Jumanne unatarajiwa kujadili hatua za kuulinda uchaguzi wa Novemba 8 uliokipa ushindi chama tawala, pamoja na kuhakikisha kiongozi wake Aung San Suu Kyi anaachiliwa huru na wenzake kadhaa waliokamatwa na jeshi.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephen Dujarric amesema umoja huo umeshindwa kuwasiliana na maafisa wa kijeshi wa Myanmar wala viongozi waliowakamata.
Dujarric ameongeza kwamba mapinduzi hayo yanaweza kuifanya hali kuwa mbaya zaidi kwa Warohingya 600,000 waliobakia katika jimbo la Rakhine.
"Kuna takriban Warohingia 600,000 waliobakia katika jimbo la Rakhine, pamoja na watu 127,000 walio kwenye kambi. Hawawezi kuondoka na hawana hata huduma za msingi za afya na elimu. Kwa hivyo hofu yetu ni kwamba tukio hili linaweza kufanya hali kuwa mbaya zaidi kwao," amesema Dujarric.
Kufuatia kampeni ya kijeshi ya mwaka 2017, Waislam wa kabila ya Rohingya wapatao 700,000 walilikimbia jimbo hilo la Rakhine na kwenda Bangladesh, ambako bado wamekwamba kwenye kambi za wakimbizi.
Mkuu wa jeshi akabidhiwa madaraka
Guterres pamoja na mataifa ya Magharibi wameimeishutumu Myanmar kwa mauaji ya utakaso wa kikabila madai ambayo taifa hilo inayakana.
Soma zaidi: Ulaya yaungana dhidi ya mapinduzi ya kijeshi Myanmar
Wanajeshi wa Myanmar walifanya mapinduzi hayo jana Jumatatu na kuchukua madaraka ya nchi kutoka serikali iliyochaguliwa kidemokrasia ya Aung San Suu Kyi, ambaye alikamatwa pamoja na viongozi wengine wa kisiasa.
Jeshi la Myanmar limesema limemzuia Suu Kyi na wenzake kwa sababu ya undangayifu uliofanyika kwenye uchaguzi. Na badala yake kukabidhi madaraka kwa mkuu wa jeshi Min Aung Hlaing na kutangaza hali ya dharura kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Dujarric amesema Umoja wa Mataifa umetoa mwito wa kuachiliwa huru mara moja wale wote waliokamatwa. Ameongeza kwamba mjumbe maalumu wa Guterres Myanmar, Christine Schraner Burgener, anafuatilia hali inavyoendelea na huenda akawa miongoni mwa watakaozungumza katika mkutano wa Jumanne wa baraza la usalama.
Vyanzo: rtre, ap